Njia ya uhakika ya kushindwa kwenye zama tunazoishi sasa, ni kutokujitofautisha, kama unafanya kile ambacho umezoea kufanya, ambacho ndiyo kila mtu pia anafanya, nafasi yako ya mafanikio ni finyu sana.
Hii ni kwa sababu wafanyaji ni wengi sana zama hizi, na watu hawatakuja kwako kwa sababu wewe unafanya au kwa sababu wanakuonea huruma. Bali watakuja kwako pale utakapokuwa na kitu cha tofauti, pale wanapopata kile ambacho hawawezi kukipata kwingine popote.
Hivyo jukumu lako la kwanza kabisa ili kufanikiwa, ni kujitofautisha kabisa na wengine, kufanya vitu vya kipekee ambavyo havijazoeleka na watu wanavihitaji sana ili maisha yao yaweze kuwa bora zaidi.
Ipo mbinu moja ambayo ukiitumia utaweza kufanya kazi ya kipekee na itakayokutofautisha kabisa na wengine.
Mbinu hiyo ni kujiamini kwamba unaweza na uko vizuri, kujiamini kwamba unao uwezo wa kufanya vizuri chochote unachofanya na kuweza kutoa matokeo bora sana kwa wengine. Unahitaji kuamini kwamba kile unachofanya kitaboresha zaidi maisha ya wengine. Na ukishakuwa na imani, hupaswi kuwa na mashaka, badala yake unapaswa kutekeleza.
Kwa kujiamini hivyo, hutawaiga wengine na wala hutajilinganisha na mwingine yeyote. Hivi ni vitu viwili vinavyowaangusha wengi, hasa wale wasiojiamini, wale wanaoona wanachofanya wengine ndiyo sahihi zaidi na hawapaswi kufanya tofauti.
Usipowaiga wengine, utafanya kile ambacho umepanga kufanya na kukifanya kwa njia bora zaidi, kwa sababu kinachofanywa na wengi huwa siyo bora. lakini utakachofanya wewe, kitakuwa bora zaidi.
Pia unapoacha kujilinganisha na wengine, unatumia vizuri uwezo mkubwa uliopo ndani yako, unaweza kufanya zaidi kwa sababu unajipima kwa ndani na siyo kwa nje. Na kila mtu anao uwezo wa kufanya zaidi, kama ataangalia ndani yake na siyo nje.
Jiamini, usiige na usijilinganishe na yeyote, kwa kuzingatia haya, utaweza kufanya kazi bora na ya kipekee sana, kazi itakayowavutia wengi na kukuwezesha kufanikiwa zaidi. Lakini usisahau kuendelea kujifunza kila siku ili kuwa bora zaidi na zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,