Viongozi wakubwa wanapofariki dunia, huwa wanajengewa minara ambayo inawakumbusha watu kuhusu viongozi hao. Minara hiyo inakuwa kumbukumbu kwa yale makubwa ambayo wameyafanya.

Kama wewe unataka kuacha kumbukumbu kubwa hapa duniani, na huna nafasi ya kujengewa mnara, basi ipo njia moja ya uhakika kwako kuacha mnara ambao watu wataendelea kuukumbuka mara zote.

Njia hii ni kujijengea tabia bora sana, tabia za kipekee, tabia ambazo kwa binadamu wa kawaida siyo rahisi. Fanya kazi ambayo ni bora sana na kuwa mfano mkubwa sana kwa wengine. Ishi kwa namna ambayo kila mtu atasema mtu huyu anaishi kwa usahihi.

Chochote unachofanya, kifanye kwa usahihi kabisa, kuwa na msimamo unaoendesha nao maisha yako na fuata msimamo huo. Kuwa na hekima, ujasiri, haki na kujidhibiti wewe mwenyewe kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako.

Kwa kuacha mnara huu muhimu sana unaojengwa kwa tabia, utawafanya watu waseme kwa nini fulani siyo maarufu, anastahili kuwa maarufu. Wewe unakuwa hufanyi kwa umaarufu, bali unafanya kwa sababu ni kitu sahihi kwako kufanya.

Uzuri wa kujijengea mnara huu wa tabia ni kwamba mnara utaanza kuonekana hata kabla hujaondoka hapa duniani. Kadiri unavyojenga tabia imara, ambazo kibinadamu zinaonekana haziwezekani, utakuwa mfano mkubwa sana kwa wengine. Wengine watafikiri kwamba huenda wewe siyo binadamu wa kawaida, au una nguvu ambazo siyo za kawaida.

Na hili ni rahisi sana kaama utaishi kwa msingi wetu muhimu wa mafanikio, NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA. Ishi kwa msingi huu kila siku, na kazana kupiga hatua zaidi kila siku, na kwa hakika, mnara utakaouacha hapa duniani hautakuwa mnara mdogo.

Jijengee tabia bora na misimamo mizuri ambayo itawafanya watu wakuone wewe ni wa tofauti kabisa na binadamu wengine. Huu utakuwa mnara ambao umeuacha hapa duniani na watu wataendelea kuuona hata kama hutakuwepo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha