Kila mtu ni mzuri sana kwenye mipango, kuweka malengo na mipango ni rahisi, na kila mtu anaweza kufanya hivyo.

Lakini inapokuja kwenye utekelezaji, ni wachache sana ambao wanaweza kutekeleza. Wengi hawaanzi kabisa, na wale wanaoanza, huwa hawafiki mbali. Ndani ya muda mfupi wanakata tamaa au wanaacha tu.

Kama hili limekuwa linakusumbua, unapanga vitu lakini utekelezaji unakuwa mgumu, kuna njia moja ya uhakika ya kukuwezesha wewe kufanya kila unachopanga.

Njia hiyo ni kutengeneza njia ya kukuwajibisha kwenye utekelezaji wa kile unachopanga.

Iko hivi rafiki, kama utajiwekea malengo na mipango yako wewe mwenyewe, tena kwa kufikiria tu wakati unajisikia vizuri, nafasi ya wewe kutekeleza ni ngumu sana. Kama utaenda hatua ya mbele zaidi, kwa kuyaandika malengo hayo, na kuendelea kujikumbusha kwa kuandika kila siku, nafasi ya kutekeleza inaongezeka zaidi.

Lakini kama unataka nafasi ya kutekeleza iwe kubwa zaidi, basi njia bora ni kuwa na mfumo wa uwajibikaji kwa mipango yako. Hapa unakuwa na mtu na mtu ambaye anakusimamia kwenye kile unachofanya, mtu ambaye hatakuruhusu uache kirahisi.

Mtu huyu atakukumbusha pale unapotoka kwenye lengo, atakuamsha pale unapoanza kusahau lengo na atakufuatilia mpaka ufikie lengo.

Kama umekuwa unasumbuka kufikia malengo unayopanga, tafuta mtu ambaye hatakuachilia kirahisi na akusimamie kwenye malengo hayo. Mtu huyu atakuwajibisha na kukusukuma zaidi, hata kama mambo yanaonekana ni magumu.

Hii ndiyo sababu wachezaji wote, licha ya kwamba wengine ni wachezaji bora, bado ni vigumu kwao kufanya mazoezi peke yao, wanahitaji kuwa na mtu wa kuwawajibisha kulingana na ufanyaji wao wa mazoezi, na hapo ndipo wanapokuwa na makocha wa kuwafundisha na kuwasimamia.

Kadhalika kwenye maisha yako, unapaswa kuwa na kocha anayekusimamia kwa karibu kwenye yale unayoyafanya ili uweze kufanikiwa zaidi. Bila ya kocha, utajikuta unahangaika na vitu vingi na hakuna kinachofanikiwa.

Kuwa na mfumo wa kukuwajibisha wewe kwenye malengo na mipango ambayo umejiwekea na hilo litakusaidia sana kufikia malengo na mipango uliyojiwekea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha