Kuna kitu kimoja kidogo sana ambacho kinawatofautisha wale wanaofanikiwa sana na wale wanaoishi maisha ya kawaida na hata kushindwa.

Kitu hicho ni eneo lipi wameweka mkazo wao kati ya matokeo na mchakato.

Watu wa kawaida, wale ambao hawajafanikiwa, huwa wanaweka mkazo wao kwenye matokeo, huwa wanaangalia nini wanapata na kujaribu kuyafanya matokeo yawe kama vile wanavyotaka wao. Sasa kwa sababu hakuna anayeweza kudhibiti matokeo, huwa wanashindwa kuyapata matokeo hayo na kubaki kuwa na maisha ya kawaida na hata ya kushindwa.

Watu wanaofanikiwa, wale ambao wanapiga hatua kubwa kwenye maisha yao, huwa wanaweka mkazo wao kwenye mchakato, huwa wanaangalia ni nini wanachopaswa kufanya ili kupiga hatua zaidi. Wanajua kitu pekee wanachoweza kudhibiti ni mchakato na kama mchakato utaenda vizuri basi matokeo yoyote yatakayopatikana yatakuwa bora kwao.

Wale waliofanikiwa hawakazani kudhibiti matokeo, kwa sababu wanajua hilo halipo ndani ya uwezo wao, bali wanakazana kudhibiti mchakato, zile hatua ambazo wanachukua kila siku. Kadiri mchakato unavyokuwa bora, kadiri wanavyofanya kitu sahihi kwa wakati sahihi, ndivyo wanavyopata matokeo bora zaidi kwao.

Pia unapokazana na mchakato, unakuwa na hatua za kuchukua kila wakati, lakini ukikazana na matokeo, unajikuta unakata tamaa, hasa pale unapotegemea matokeo makubwa na unaanzia chini.

Rafiki, hakuna kitu chochote unachoweza kudhibiti kwenye maisha, isipokuwa wewe binafsi, unaweza kujidhibiti wewe tu, vingine vyote vipo nje ya uwezo wako. Sasa kwa sababu mchakato ni wewe unaufanyia kazi, kama unaweza kujidhibiti pia unaweza kudhibiti mchakato.

Una udhibiti kwa fikra zako, mitazamo yako, tabia zako, kujali kwako na hata kujitoa kwako. Kama utaweka nguvu kwenye hivi, kisha kuona jinsi ambavyo vinaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi, kidogo kidogo maisha yako yanakuwa bora zaidi kila siku.

Kazana na mchakato, usipoteze muda wako kukazana kudhibiti matokeo, wewe weka juhudi, fanya kila kinachopaswa kufanya, kisha pokea matokeo unayoyapata, baada ya hapo, kazana kuwa bora zaidi. Hivi ndivyo watu wanavyotengeneza mafanikio makubwa kwenye maisha yao, na wewe pia utatengeneza mafanikio makubwa kwa kuzingatia mchakato na siyo matokeo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha