Michezo yote ambayo tunajihusisha nayo, huwa ina namna ya kupima ushindi, na ushindi ndiyo kila anayeshiriki mchezo anapigania. Na ipo hali fulani ya furaha na kujiamini ambayo mtu huwa unaipata pale unapopata ushindi kwenye mchezo unaocheza. Hata kama huchezi, kwa kuwa shabiki tu wa upande ulioshinda, unakuwa kwenye hali ya furaha.

Sasa upo mchezo ambao hata ukishinda, haukupi furaha. Mchezo huu watu huwa wanapenda kujihusisha nao, na mara nyingi wanashinda kwa sababu wanaweka nguvu nyingi sana kwenye kushinda mchezo huo, lakini baada ya kushinda, bado wanakuwa wanajisikia vibaya sana.

Mchezo ninaozungumzia hapa ni hofu, pale unapokuwa na hofu juu ya kitu fulani, kwa kuogopa kuchukua hatua kwa sababu matokeo fulani mabaya yatatokea. Kisha unajisukuma kuchukua hatua na kweli yale matokeo uliyokuwa unahofia yanatokea, unakuwa umepatia kwenye mchezo wako, kimchezo unakuwa umeshinda, lakini kwa hali ya kawaida, unajisikia vibaya kwa kupata matokeo ambayo hukuyategemea.

Kuwa na hofu ni sawa na kucheza kamari kwa kujitabiria kushindwa, na kweli unashindwa, kitu ambacho hakitakupa furaha.

Rafiki, shiriki mchezo ambao ushindi wake utakupa furaha, ushindi wake utakupa hamasa ya kupiga hatua zaidi. Hivyo achana kabisa na hofu zozote ulizonazo.

Kwenye lengo kubwa unalokuwa unalifanyia kazi, ligawe kwenye malengo madogo madogo sana, ambayo unaweza kuyakamilisha bila ya shida. Na kila unapokamilisha lengo dogo, furahia na jipongeze, hiyo itakupa hamasa ya kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Kwa kuwa na ushindi mdogo mdogo ambao unaukusanya kila siku, unajiweka kwenye nafasi ya kupata ushindi mkubwa zaidi.

Shiriki mchezo au mashindano yako mwenyewe, ambayo ushindi wake unakupa furaha na hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Kaa mbali na hofu, kila hofu inapokuingia iondoe haraka kwa kufikiria picha ya mafanikio makubwa unayofanyia kazi na kufikiria lengo dogo unalolifanyia kazi kwenye siku yako.

Roma haikujengwa kwa siku moja, safari ya maili elfu moja huwa inaanza na hatua moja na mafanikio yako makubwa kwenye maisha, yanaanza na ushindi mdogo mdogo unaoweza kuukusanya kila siku kwenye maisha yako.

Zingatia sana hili kwenye kila siku unayoishi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha