Moja ya kosa kubwa sana ambalo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya na linawagharimu, ni kufikiria zaidi matatizo yao binafsi kuliko wanavyofikiria matatizo ya wateja.

Wengi hujisahau na kufikiri kwamba mteja amekuja kununua kwa sababu wao wanauza, kitu ambacho siyo sahihi.

Mteja haji kununua kwako kwa sababu wewe unauza, au kwa sababu una uhitaji mkubwa wa fedha.

Mteja anakuja kununua kwako kwa sababu ana matatizo, ana uhitaji, ana changamoto ambazo anahitaji kuzitatua ili maisha yake yaweze kwenda vizuri.

Kwa kifupi, kinachomfanya mteja aje kununua kwako, ni matatizo yake na siyo matatizo yako wewe unayeuza.

Hivyo basi, katika kuwasiliana na mteja wako, katika kuongea na mteja na katika kumshawishi anunue, unapaswa kuegemea zaidi kwenye matatizo yao na siyo matatizo yako.

Pata nafasi ya kujua matatizo waliyonayo, yanayowasukuma kutaka kununua unachouza, kisha wape maelezo mazuri ya jinsi wanachotaka kununua au unachowashawishi wanunue kitawasaidia kutatua matatizo hayo.

Kuwa na mazungumzo na mawasiliano bora na wateja wako, kwa kujadili vitu ambavyo ni muhimu zaidi kwao, vitu ambavyo wanavijali zaidi.

Pia unaweza kuwahoji zaidi kuhusiana na tatizo au hitaji walilonalo, na muhimu zaidi, unaweza kuwauliza kama wanataka suluhisho la kitu fulani ulichokiona kwao, ambacho labda kwa sasa hawakiangalii kwa ukaribu zaidi.

Kadiri unavyoongea na wengi zaidi, kadiri unavyojadili kwa kina matatizo yao na kuwapa suluhisho, ndivyo unavyopata fursa nyingi zaidi za kuuza kwa wateja wako.

Chukua muda wako kuongea na watu wengi na wapya zaidi kuhusu matatizo yao, na siyo kuongea na watu wale wale ambao tayari umeshawazoea kila siku.

Kama unataka kupata wateja wapya na wengi kwenye biashara yako, lazima pia uzungumze na watu wengi wapya. Na nimeshakuambia kipi cha kuzungumza nao, matatizo yao, na siyo yako.

Unapojipa nafasi ya kuongea na mtu na ukawa msikilizaji mzuri, haitakuchukua muda kabla hujajua matatizo, changamoto au wasiwasi ambao mtu anakuwa nao. Hitaji jingine muhimu ni hilo la kuwa msikilizaji mzuri, litakusaidia kuijua shida hasa na kuweza kujua njia za kuitatua.

Rafiki, jikumbushe hili kila mara, ni matatizo ya mteja ndiyo kipaumbele chako cha kwanza inapokuja kwenye biashara na siyo matatizo yako binafsi. Hayo yaweke pembeni kwanza unapokuwa upo kwenye biashara.

Na uzuri ni kwamba, kwa sheria ya asili, unapokazana kutatua matatizo ya wateja wako, matatizo yako nayo yanatatuka moja kwa moja bila hata ya kutumia nguvu kubwa. Lakini ukikazana na matatizo yako pekee na kupuuza ya wateja, unayafanya kuwa makubwa zaidi na kuwapoteza wateja.

Ni matatizo ya mteja ndiyo yanapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye biashara yako, na siyo matatizo yako binafsi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha