Wafanyabiashara wavivu, wale wasiotaka kuweka kazi kwenye biashara zao lakini wanaotaka kupata wateja wengi na mafanikio makubwa, huwa wana njia waliyozoea kutumia.
Njia hiyo ni kuwa na bei rahisi kuliko wafanyabiashara wengine. Kushusha zaidi bei ili kuwavutia wateja kununua kwao. Njia hii huwa inaweza kuleta matokeo mazuri ndani ya muda mfupi, lakini kwa muda mrefu huwa ni majanga makubwa.
Kwa muda mfupi wateja wataongezeka kweli, kwa sababu watu wengi wanapenda vitu vya bei rahisi. Lakini kadiri bei inavyokuwa chini, ndivyo faida nayo inapungua. Unakuwa na wateja wengi lakini faida ni kidogo, hivyo unashindwa kuwahudumia vizuri. Huduma zinakuwa mbovu, wateja wanakata tamaa na kuondoka.
Kitu kingine kinachofanya njia hii iwe na changamoto baadaye ni kadiri bei inavyokuwa rahisi, unakuwa umewavutia wale wanaonunua kwa kuangalia bei tu na siyo kujali. Sasa hawa ni wateja ambao hawajali chochote kuhusu wewe na biashara yako ila bei.
Upo mbadala wa bei rahisi, mbadala utakaokuwezesha kuwa na wateja wengi, wateja ambao ni bora kwako na wapo tayari kulipa bei ambayo umeiweka, bei ambayo itakupa wewe faida na kukuwezesha kutoa huduma bora kabisa kwenye biashara yako.
Mbadala wa bei rahisi ni kujali kuhusu wateja wako, kufanya kitu cha tofauti ambacho hakuna mwingine anayefanya, kuwa mtu ambaye mteja anaweza kukutegemea, kuwa mtu unayeaminika, kwa kutekeleza kila unachoahidi, kile unachouza kuwa rahisi kutumika kwa wateja wako na kuendelea kuwasaidia hata baada ya kuwa umewauzia na mwisho kuwa rafiki wa wateja wako, wataja wanaona kuja kwako siyo tu kuja kununua, bali kuja kukutana na wewe rafiki yao.
Kama umepanga kukaa kwenye biashara kwa muda mrefu, na hapa nazungumzia miaka zaidi ya hamsini, basi jua njia za mkato kama kupunguza bei hazitakufikisha mbali. Badala yake unahitaji kutumia njia zinazoweza kwenda na wewe mbali. Na njia bora za kutumia ni hizo tulizoshirikishana hapa.
Chagua kuwa chochote ambacho kinaongeza thamani kwa mteja wako, lakini kamwe usichague kuwa muuzaji wa bei rahisi kuliko wote, kwa sababu utawavutia wateja wanaotaka rahisi, na hawa ni wateja ambao wanaweza kukusumbua sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,