Kujenga mahusiano bora, hasa yale ya karibu zaidi kama mahusiano ya ndoa au mahusiano ya kifamilia inahitaji kazi.
Kujenga mahusiano bora siyo kitu rahisi kama wengi wanavyofikiri, siyo kitu kinachotokea tu bali ni kitu kinachofanyiwa kazi hasa.
Upo mchezo mmoja hatari sana ambao wengi wamekuwa wanaufanya kwenye mahusiano. Mchezo huu umekuwa unaharibu na kuvunja mahusiano mengi, lakini bado watu hawajifunzi na kuachana na mchezo huu.
Mchezo huo hatari unaoharibu mahusiano mengi ni kutaka kuwa sahihi mara zote.
Kutaka kuwa sahihi mara zote au kutaka kumshinda mwenzako mara zote ni mchezo hatari sana kwenye mahusiano. Ni mchezo hatari kwa sababu hata kama utashinda kwa kujiamini umekuwa sahihi, bado utakuwa umeshindwa.
Kwa sababu kwenye mahusiano unaweza kushinda kwa maneno, lakini mwenzako akawa ameumia kihisia na hilo likapelekea mahusiano kuzorota zaidi.
Kama lengo lako kwenye mahusiano ni kuwa sahihi mara zote, ni kutaka kumwonesha mwingine kwamba yeye amekosea na wewe ndiyo upo sahihi, kama unataka mwenzako aone jinsi ambavyo wewe upo makini na yeye ni mzembe, utajifurahisha kwamba umemwonesha kitu, lakini utakuwa umemweka mbali zaidi.
Kitu kingine kibaya zaidi kwenye mahusiano ni kukusanya makosa mengi na baadaye kuyatumia kama njia ya kulipa. Pale mnapokosana kwa kitu kidogo unaanza kukumbushia kila aina ya makosa ya nyuma. Kuhesabu na kutunza makosa kwa namna hii ni kitu kingine kinachoharibu sana mahusiano.
Kama nilivyosema wakati tunaanza hapa, mahusiano yanahitaji kazi sana kuyajenga. Siyo lazima mara zote uwe sahihi, wakati mwingine inabidi ukubali kuweka usahihi wako pembeni ili kuyajenga na kuimarisha mahusiano yako.
Pia siyo lazima mtu akiri kila aina ya makosa ndiyo ukubaliane naye, wakati mwingine mtu anaweza kuwa amejutia makosa yake, lakini unavyorudia kuyakumbushia kila mara inamfanya aone ni sahihi kwake kufanya hivyo.
Usikazane kushinda kwenye ubishi au kwenye kuonesha nani yupo sahihi na nani anakosea, halafu ukaishia kuharibu mahusiano yako.
Mahusiano bora yanajengwa kwa kujali, kusikilizana, kuchukuliana, kusameheana na kuwa tayari kusahau makosa ya wengine hata kama ni makubwa kiasi gani.
Kazana kuyaboresha maisha yako kwa kuachana kabisa na mchezo wa kutaka ushindi mara zote na kuwafanya wengine waone wanakosea mara zote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika umenikumbusha mengi, sasa tatizo kwa maisha ya sasa unaweza kukuta maisha ni mwanamke/mwanaume kila siku, wiki, mwezi, mwaka ni wa kuna au kukumbushia yaliyopita, nilichojifunza ukiona inaanza kuwa hivyo tafuta msaada mapema usichukulie kirahis au kimazoea, maana wengine tumeumia na kuvunja mahusiano kwa kupitia hayo kutoyapa umakini wake.
LikeLike
Ni kweli kabisa Beatus, kadiri unavyochukua hatua mapema, ndivyo unavyopunguza matatizo makubwa baadaye.
LikeLike