Asili ni kama inatutega, kama inatupa ushawishi tusifanye yale ambayo tunapaswakuyafanya.

Chukua mfano wa shamba, kuwa na shamba zuri na lenye rutuba na mvua zipo, yataota magumu mengi, ambayo hayana hata matumizi. Hapo hujalima wala kufanya chochote, yanaota magumu na yanaota vizuri. Kwa nini yasingeota mazao ambayo wewe unayahitaji?

Hapa ndipo unapogundua ya kwamba kila kitu chenye thamani kwenye maisha kinahitaji kazi, na kama kazi haitawekwa, kuna vitu vingine vitakavyotokea, ambavyo havitakuwa bora.

Na hili ndiyo linalotokea pale tunapopanga kufanya kazi fulani, inakuwa rahisi sana kutokufanya kazi hiyo kuliko kuifanya.

Chukua mfano umepanga kuandika, au kusoma kitu au hata kutekeleza majukumu mengine yenye manufaa kwako. Itakuwa rahisi sana kwako kufanya vitu vingine vyote kuliko kutekeleza jukumu kuu. Itakuwa rahisi kwako kupangilia vitu ambavyo hata hukuwa na ratiba ya kuvipangilia, itakuwa rahisi kutembelea mitandao ya kijamii, itakuwa rahisi kuwasiliana na wengine. Na itakuwa rahisi kusema nitafanya kesho au wakati mwingine.

Pale unapoamua kikubwa cha kufanya, mambo mengine yote yanakuwa rahisi kufanya lakini siyo kile kikubwa. Unapaswa kulielewa hili maana ni sawa na magumu yanayoota shambani. Unaweza kujikuta umetingwa, siku inaisha na unakuwa umechoka, lakini ukiangalia hakuna kikubwa ulichofanya.

Unapopanga kufanya kitu, ambacho ni kikubwa na chenye maana, unapaswa kuweka sababu zote pembeni na kukifanya. Hata kama kitajitokeza kitu kingine rahisi kiasi gani kufanya, usikubali kikuondoe kwenye kile muhimu ulichopanga kufanya. Unapaswa kufuata mpango wako kama ulivyoweka na kuwa makini na yale yanayotokea pembeni yanayokushawishi uache unachofanya na uyafanye.

Maisha yetu ni kama shamba au bustani, mazao ni zile kazi zetu, na mengine yote yanayotuzonga ni magugu. Kama hutakuwa makini na kuondoa magumu mara kwa mara, utashangaa maisha yako yamejaa magumu na hakuna mazao yoyote unayozalisha. Ni rahisi kwa magugu kuota shambani kuliko ilivyo rahisi kwa mazao kuota.

Ondoa kila aina ya magugu kwenye maisha yako na usiyape nafasi kabisa, kila yanapoanza kujitokeza yaondoe mara moja. Kwa kuondoa magumu unaacha nafasi ya kazi muhimu kufanyika na kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha