Ni hisia zako, hisia zako ndiye adui namba moja kwenye uwekezaji wako.
Pia hisia zako kama hutaweza kuzidhibiti, zitakuwa adui wako wa kwanza kwenye mafanikio yako.
Hisia kuu mbili zinazowavuruga wengi kwenye uwekezaji ni hofu na tamaa.
Wakati ambapo fursa ya kuwekeza zaidi inapatikana, watu huwa wanatawaliwa na hofu wakiona kuweka fedha zinaweza kupotea, hivyo hawawekezi.
Wakati ambapo ndiyo muda mzuri wa kuuza uwekezaji mtu apate faida mtu anaingiwa na tamaa, kwa sababu uwekezaji unakuwa unafanya vizuri basi anajua hayo mazuri yataendelea na akiuza atakosa faida kubwa. Kinachotokea ni fursa hiyo ya kuuza kwa faida inapita na mtu anakuwa hajauza.
Hata kwenye maisha ya kawaida, hofu na tamaa vimekuwa adui mkubwa kwa wengi kupiga hatua. Wengi wamekuwa wanakutana na fursa nzuri sana kwao kupiga hatua, lakini wamekuwa wanasita kuchukua hatua kwa sababu ya hofu, kwa kuwa hawana uhakika wa kupata matokeo waliyotaka, hawachukui hatua.
Kwa upande wa pili mtu anaweza kuwa kwenye kitu ambacho kinafanya vizuri, lakini kinabadilika, yeye kwa tamaa ya kuendelea kupata, habadiliki, anaendelea kung’ang’ana na njia za awali alizozoea. Inafika wakati mabadiliko yamekuwa makubwa sana kiasi kwamba njia za awali hazifanyi tena kazi, na hapa mtu anakuwa ameachwa nyuma na hawezi kunufaika tena.
Kila wakati jichunguze kama hisia hizi mbili hazikusukumi kufanya maamuzi ambayo yanakuzuia kupiga hatua zaidi. Kila unapoacha kufanya kitu, jiulize je hakuna hofu ambayo imejificha nyuma ya maamuzi hayo?
Na kila unapokimbizana na fursa mpya kila wakati, jiulize je ni fursa umeiona kweli au ni tamaa yako ya kupata haraka? Kwa sababu kitu ambacho kimekuwa kinapelekea wengi kuibiwa na kutapeliwa ni tamaa. Hata wale ambao wanawatapeli wengine, wanajua watu wana tamaa, hivyo wakiwapa hadithi kwamba watanufaika zaidi, watakuwa tayari kutoa chochote wanachowaambia watoe.
Dhibiti sana hisia zako kama kweli unataka kupiga hatua, mara zote hakikisha maamuzi unayofanya yametokana na fira sahihi ambazo umekuwa nazo. Kama huna uhakika ni fikra au hisia zimekusukuma, jipe muda kidogo na tafakari kwa kina kila kilichokufikisha kwenye maamuzi ambayo umefikia.
Hisia ni adui mkubwa wa mafanikio yako, hakikisha haziwi sehemu ya maamuzi yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,