Matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha yetu, huwa tunayaandaa au kuyatengeneza sisi wenyewe.

Hata kama waliosababisha matatizo hayo ni wengine, lakini huwa hatukosi mchango wetu kwenye matatizo hayo.

Na tunachangia matatizo haya mengi kwa utumwa ambao tumekuwa nao ambao hatuujui kama ni utumwa kwetu.

Katika hali ya kawaida, huwa fikra zetu zinatusaidia katika kufanya maamuzi yote muhimu tunayohitaji kufanya, na tukiwa na utulivu tunafanya maamuzi bora sana.

Lakini katika hali isiyo ya kawaida, ambayo ndiyo hali tunayokuwa nayo wakati mwingi wa maisha yetu, huwa hatuwezi kufikiri kwa kina, na hivyo tunafanya maamuzi ambayo siyo bora.

Hali isiyo ya kawaida ninayozungumzia hapa ni pale hisia zinapokuwa juu, una furaha kupitiliza, una hasira, tamaa au umeingiwa na wivu fulani. Hizi ni hali za kawaida kwenye maisha yetu, lakini si hali za kawaida kwenye akili zetu.

Katika hali hizi za hisia, sehemu ya akili inayofikiri inakosa nguvu, na sehemu ya hisia inatawala. Hapo sasa unasukumwa na hisia kufanya maamuzi, ambayo huwa hayawi maamuzi bora, kwa sababu hisia hazifikiri, hisia zinafanya.

Kwa kutokujijua unakuta umefanya mambo ambayo baadaye ukikaa na kutulia, unajiuliza kwa nini ulifanya, ulikuwa unafikiria nini.

Swali hilo siyo sahihi na wala hutapata jibu, kwa sababu wakati unafanya ulikuwa hufikirii.

Sasa njia pekee ya kuondoka kwenye utumwa huu ni kuepuka mazingira yanayokaribisha utumwa huo, yaani mazingira yanayoamsha hisia kali ndani yako.

Kujiambia kwamba utaweza kuzituliza hisia ni sawa na kusema unaweza kuzima moto wa nyumba inayoungua kwa kufunika na blanketi, ni kujidanganya. Hisia zikishaingia, kila ni rahisi sana kujishawishi juu ya chochote na kuona ni sahihi. Lakini ni mpaka baadaye unapokuja kujigundua wakati unafanya ilikuwa sahihi sana, lakini sasa unaona siyo sahihi.

Epuka sana mazingira yanayoamsha hisia ndani yako, na hili litakuondoa kwenye utumwa wa kufanya mambo bila kufikiri na kuingia kwenye matatizo.

Njia nyingine ambayo inaweza isiwe na nguvu sana, lakini inasaidia ni kujiwekea vigezo vya kufanya maamuzi muhimu. Mfano usiwe mtu wa kufanya maamuzi na kutekeleza kwa wakati mmoja, badala yake ukishafanya maamuzi unasubiri angalau masaa 24 kabla ya kuanza utekelezaji.

Nikupe mfano, umetoka nyumbani asubuhi, hukuwa na mpango wa kununua kitu chochote, ukakutana na nguo nzuri, ulipoiangalia ukaipenda, muuzaji akajua umeipenda na akaanza kukushawishi kuinunua. Anakuambia jinsi gani itakupendeza, anaongeza namna gani huwezi kuipata kwingine tena kwa bei ile.

Sasa fikra zako zinabadilika, kutoka kwenye kutokuwa na mpango wa kununua kitu siku hiyo, mpaka kwenye kufikiria kwamba hii ni fursa pekee, hutapata kama hiyo, unajishawishi kwamba hata hivyo hujanunua nguo siku nyingi, na pia utaitumia kwenye shughuli fulani inayokuja, unatoa fedha na kununua. Unarudi nyumbani, unajiuliza ilikuwaje umenunua nguo hiyo, hata usipojiuliza, unashangaa hata huivai kwa muda mrefu.

Lakini kama ungekuwa na utaratibu kwamba unapokutana na kitu kipya cha kununua, hununui hapo hapo, badala yaake utasubiri mpaka kesho yake. Ungeondoka na huenda mpaka kufika kesho yake usingekuwa hata unakumbuka kwamba kuna nguo ulipanga kununua.

Huu ni mfano mdogo wa nguo, sasa uweke kwenye mengine unayofanya kwenye maisha yako. Ondokana kabisa na utumwa wa kufanya maamuzi kwa kusukumwa na hisia na utapunguza sehemu kubwa ya matatizo unayokabiliana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha