“Always read something that will make you look good if you die in the middle of it.” — P.J. O’Rourke
Ni upendeleo wa kipekee sana kwetu kuweza kuiona siku hii nyingine mpya na nzuri kwetu.
Hakuna kikubwa tulicholipa ili kuiona siku hii, ambacho wale ambao hawajaiona wameshindwa kulipa.
Hivyo kitu pekee tunachoweaa kulipa kwa siku hii tuliyoiona leo, ni shukrani.
Haijalishi maisha yako ni magumu kiasi gani, anza siku hii na shukrani, na dunia itafunguka kukupa kila unachotaka.
Tuiendee siku hii kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari KAMA UTAKUFA UKIWA UNAFANYA…
Mara zote, fanya kitu ambacho kama utakufa ukiwa unakifanya, basi utaonekana ni mtu mzuri, ni shujaa.
Usifanye kitu chochote ambacho kama ukifa wakati unakifanya utaacha aibu kubwa kwako.
Kama ni kusoma, soma kitu ambacho hata kama unakufa wakati unakisoma, watu wanaokukuta katika hali hiyo, wanakuheshimu, kwa namna ulivyokuwa unajipatia maarifa bora.
Usije ukafa ukiwa unasoma udaku, kuhusu maisha ya wengine na nani anatembea na nani, hata ukifa ukiwa unasoma kitu kama hicho, watu wataona ulichagua kupoteza muda wa maisha yako.
Kadhalika kwenye kazi, kama utakufa ukiwa unafanya kazi, basi iwe kazi yenye maana kwako na kwa wengine, iwe kazi ambayo itakupa heshima.
Itawafanya watu waone kweli uloyatoa maisha yako kwa vitu muhimu.
Na hili linakwenda kwenye maisha binafsi pia, chochote unachotaka kufanya, jiulize je nikifa wakati nafanya kitu hiki, kitaniweka kwenye sifa nzuri au mbaya.
Yupo mwanaharakati mmoja aliyekuwa maarufu sana duniani, aliuawa kwa kupigwa risasi, sasa waliofika eneo la tukio wa kwanza, walikuta alikuwa kwenye mawasiliano na mtu, walipofuatilia waligundua alikuwa anawasiliana na ‘mchepuko wake’, huyu ni mtu ambaye alikuwa ameona na ana familia. Hili lilimshushia heshima yake, licha ya kuwa aliendesha harakari kubwa.
Hivyo usijidanganye kwamba huwezi kufa ukiwa unafanya kitu fulani, hakuna ajuaye wakati gani anakufa.
Pia hufanyi hivyo kwa ajili ya wengine, bali unafanya kwa ajilo yako, kuweza kusimamia msimamo wako na kuishi maisha bora kwako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kitu ambacho kitakuoa heshima kama utakufa wakati unakifanya. Vingine vyote achana navyo.
#AmkaKwaShukrani, #FanyaKilichoMuhimu, #MudaNiMali, #SimamiaMisingiYako
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha