Rafiki, unajua nimekuwa nakataza kabisa usisumbuke na njia za mkato za kufika kwenye mafanikio makubwa.

Zile njia ambazo zinakuahidi mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi bila ya kufanya kazi kabisa.

Zile njia ambazo zinakuambua hutafanya kazi kwa nguvu bali utafanya kwa akili.

Hizo ni njia ambazo zimewaumiza wengi, wengi wamelaghaiwa na kutapeliwa kwa njia hizo na kushindwa kabisa.

Rafiki, ninachotaka kukuambia leo, ipo njia halali ya mkato ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Njia hii inakuepusha kufanya makosa ambayo yanakugharimu au kukupotezea muda wa wewe kuweza kupiga hatua kubwa.

Njia hiyo ni kujifunza kupitia wengine waliofika pale unapotaka kufika wewe. kila aliyefika unakotaka kufika, yapo mengi aliyofanya kwenye safari yake. Yapo makosa makubwa aliyofanya, ambayo kwa wewe kuyajua na kuyaepuka utapunguza muda na nguvu ambazo ungepoteza kwenye makosa hayo.

Pia yapo mazuri ambayo anakuwa ameyafanya ambayo ukiyajua na kuyafanya yatarahisisha zaidi safari yako.

Jifunze sana rafiki, wachague wale waliofika pale unapotaka kufika wewe, kisha jifunze kila kitu kuhusu wao. Jifunze namna walivyofanya mambo yao, namna walivyoamini, na mna walivyofikiri na kila kitu.

Zama ndani kwa kujifunza kila kitu kuhusu mtu mmoja au wawili na kisha kufanyia kazi yale unayojifunza ili uweze kuokoa muda na nguvu zako zisipotee kwa kurudia makosa ambayo wengine wamefanya.

Kuwa makini usijifunze kwa wengi sana, maana mafunzo yataanza kukinzana na hutajua lipi ni sahihi na ufanyie kazi.

Pia kuwa makini usiwe mtu wa kuiga maisha ya wengine, kwa sababu pamoja na kutaka kufika walipofika wao, bado wewe unatofautiana kabisa na wao, hivyo ishi uhalisia wako.

Na mwisho siyo lazima unayejifunza kwake awe hai au karibu yako, anaweza kuwa mtu ambaye aliishi siku za nyuma sana, lakini kazi zake bado zipo na hivyo kujifunza kupitia kazi zake.

Na kama ni mtu aliye karibu, ambaye unaweza kumfikia, basi jifunze kila kitu kuhusu yeye.

Uzuri ni kwamba watu wengi wamenadika sana kuhusu maisha yao, kushirikisha yale waliyojifunza na hatua walizopiga, hivyo una wigo mpana sana wa kujifunza na kuweza kupiga hatua.

Lazima uwe na mtu mmoja au wawili, na wasizidi watatu ambao unajifunza kutoka kwao, hawa watakusaidia usipoteze muda kwenye safari yako ya mafanikio kwa kujaribu vitu ambavyo vitakupelekea kushindwa kama walivyoshindwa wao.

Mtu mmoja alisema kujifunza kutokana na makosa yako mwenyewe ni ujinga, kujifunza kutokana na makosa ya wengine ni hekima. Kuwa na hekima na kwa hakika itafupisha safari yako ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha