Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 50 la mwaka huu 2018 siyo rafiki yetu tena, tayari linatuacha, huku pia mwaka 2018 ukiwa unatuaga kabisa.

Ni imani yangu juma namba 50 limekuwa bora sana kwako, limekuwa juma la kuchukua hatua kubwa na kuweza kupata matokeo bora au kujifunza. Kumbuka kwenye safari ya mafanikio unashindwa pale tu unapokata tamaa, kama bado hujakata tamaa, kikwazo chochote unachokutana nacho ni darasa kwako, la kujifunza namna bora zaidi ya kufanya ili kufanikiwa.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA hili la 50, ambapo nimekuandalia maarifa mazuri na bora sana kwako kuweza kupiga hatua ili kupata matokeo bora sana kwenye maisha yako. Jifunze mambo haya kwa kina, yatafakari jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yako, kisha chukua hatua. Kumbuka hakuna kitu kitakachofanya kazi kama wewe mwenyewe hutafanyia kazi yale uliyojifunza.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Moja kwa moja tuingie kwenye tano za juma namba 50;

#1 KITABU NILICHOSOMA; TABIA 33 ZA WAJASIRIAMALI WENYE MAFANIKIO MAKUBWA.

Kama ipo njia ya mkato ya kufanikiwa, basi ni kuangalia wale waliofanikiwa wanafanyaje mambo yao na kufanya kama wao. Na sehemu ya kwanza kuiga ni tabia za wale waliofanikiwa.

Waandishi Steve Scott na Rebecca Livermore kupitia maisha yao binafsi na ya wajasiriamali wenye mafanikio makubwa, wametushirikisha tabia 33 ambazo wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wanaziishi kila siku.

Kwa wewe kuzijua na kuziishi tabia hizi, utaweza kutatua changamoto kubwa ambazo ndiyo zinazowazuia wengi kufanikiwa.

Waandishi wanasema wajasiriamali wote wanakabiliwa na changamoto kuu tano;

Moja; kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.

Mbili; kushindwa kukamilisha waliyopanga kufanya.

Tatu; ushindani kuwa mkali.

Nne; mahusiano mabovu ya kibiashara.

Tano; msongo na uchovu.

Changamoto hizi tano zimekuwa kikwazo kwa wajasiriamali wengi kukua na kufikia ndoto zao. Waandishi wanatuambia kama tutaziishi tabia hizi 33 wanazotushirikisha, na kuzifanya kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku, tutaweza kuvuka vikwazo hivyo vitano.

Karibu sasa tujifunze tabia 33 za maisha ya kila siku ya wajasiriamali wenye mafanikio makubwa.

  1. Anzia sokoni, wengi huanza kufanya kitu kwa mapenzi yao wenyewe na siyo mapenzi ya soko. Kama unataka kufanikiwa, anza kujua watu wanataka nini kisha wape hicho wanachotaka.
  2. Usiogope kushindwa, kabla hujafanikiwa, utakutana na vikwazo na changamoto mbalimbali, utashinda kwenye mengi, lakini kama hutakata tamaa, mwishowe utashinda.
  3. Gundua fursa zilizojificha kwenye majanga mbalimbali. Unapokutana na majanga au changamoto, usiangalie upande wa matatizo, badala yake jiulize ni fursa gani iko hapa, na utaziona fursa nyingi zilizojificha kwenye majanga.
  4. Toa thamani kubwa kwa wateja wako, wateja wataendelea kununua kwako kama kuna thamani wanaipata. Hakikisha mteja hakusahau kabisa, kwa namna unavyompa thamani ya kipekee.
  5. Amka asubuhi na mapema, hii ni tabia moja ambayo itakupa ushindi mkubwa sana kwenye siku yako. Unapoamka mapema kuliko wengine na ukatumia muda huo kwa maandalizi na kufanya yaliyo muhimu, utaweza kupiga hatua sana.
  6. Tenga muda wako na fanya jambo moja kwa wakati. Watu wengi huwa wanafikiria kufanya mambo mengi kwa pamoja ni kuokoa muda, lakini matokeo ni kinyume, kadiri mtu anavyofanya mengi kwa pamoja, ndivyo anavyopoteza muda na umakini wake. Kama unataka kukamilisha mengi, tenga muda wako na kisha fanya jambo moja kwa wakati.
  7. Fanya mambo yanayoendana pamoja. Unapopanga ratiba ya kufanya vitu vyako, vile vitu ambavyo vinaendana, panga kuvifanya pamoja, hasa pale vitu hivyo vinapokuwa havihitaji umakini mkubwa. Kwa njia hii inakuwa rahisi kwako kukamilisha yale yanayoendana. Na hii haipingani na namba sita ya kufanya jambo moja kwa wakati, ila hapa unayaweka pamoja yale yanayoendana ili uweze kuyakamilisha.
  8. Kuwa na mapumziko ya mara kwa mara. Kazi zetu nyingi tunafanya tukiwa tumekaa, hili linaleta uchovu na pia ni hatari kiafya. Suluhisho ni kuwa na mapumziko ya mara kwa mara ambapo unasimama na kutembea kidogo au kujinyoosha kabla ya kuendelea na jukumu jingine.
  9. Kuwa na orodha mbalimbali, popote unapokuwa, kuwa na orodha unayofanyia kazi. Na unapopata wazo jipya, liandike mahali, usiamini kumbukumbu zako, utaishia kusahau mengi au kuijaza akili yako vitu visivyo muhimu kwenye kile unachofanya kwa wakati huo.
  10. Weka malengo ambayo unaweza kuyafanyia kazi, malengo yanayopimika na unayoweza kuona ni wapi unakwenda na unafikaje pale. Bila ya malengo unayoweza kufanyia kazi, hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
  11. Tumia vizuri muda wa uzalishaji mkubwa kwako. Kila mmoja wetu ana muda ambao anakuwa na uzalishaji mkubwa sana. Huu ni muda ambao akili ya mtu inakuwa inafikiri kwa umakini na mwili unakuwa na nguvu ya kutosha. Jua ni wakati gani wa siku unakuwa kwenye hali hii kisha weka yale majukumu muhimu kwenye muda huo.
  12. Pima maendeleo yako kibiashara kwenye yale maeneo muhimu. Kila biashara ina maeneo yake muhimu, ambayo hayo yakienda vizuri basi biashara inakuwa ya mafanikio makubwa. Yajue maeneo muhimu kwenye biashara yako kisha pima maendeleo yako, pima hatua unazopiga ukilinganisha na malengo uliyojiwekea. Hii ndiyo njia rahisi ya kupima hatua unazopiga.
  13. Epuka kujilisha vitu visivyo na maana. Habari, mitandao ya kijamii na kelele nyingine zimekuwa zinachukua muda wa wengi na wanashindwa kufanya yale muhimu. Epuka kujilisha vitu hivyo visivyo na maana na tumia muda wako kwa yale majukumu muhimu kwako.
  14. Tengeneza muda wa kujitenga na teknolojia. Teknolojia zinarahisisha sana maisha, lakini pia zimekuwa usumbufu mkubwa sana kwenye maisha yetu. Tenga muda ambao utajitenga na teknolojia hizi, ili uwe na utulivu unaokuwezesha kufikiri kwa kina na hata kutekeleza majukumu ambayo ni muhimu kwako, yanayohitaji utulivu wa hali ya juu.
  15. Weka mkazo kwenye uimara wako. Kuna maeneo ambayo una uimara na maeneo ambayo una udhaifu, unachopaswa kufanya ni kuweka mkazo kwenye uimara wako kuliko kukazana na madhaifu wako. Tafuta wenye uimara kwenye madhaifu wako na wape wafanyie kazi maeneo hayo.
  16. Jitofautishe na wengine. Ukifanya kile ambacho wengine wanafanya utapata wateja wa kawaida. Ukifanya kile ambacho hakuna mwingine anayefanya utapata wateja wengi na wakipekee. Unapaswa kujitofautisha kabisa na wengine ili kupata wateja wa kipekee, ambao wanakuwa mashabiki wa biashara yako.
  17. Tumia vizuri muda uliokufa kujifunza na kupiga hatua. Moja ya hitaji la kila mjasiriamali ni kuendelea kujifunza na kupiga hatua zaidi. Lakini mahitaji ya kila siku yanamfanya mtu akose kabisa muda wa kujifunza. Pamoja na majukumu mengi unayoweza kuwa nayo, bado kuna muda mwingi unaokuwa nao ambao huwezi kufanya chochote. Huu ndiyo muda uliokufa. Mfano muda unaokuwa kwenye foleni barabarani au kusubiri huduma fulani, muda unaofanya mazoezi au kufanya kazi zisizohitaji umakini mkubwa. Unaweza kutumia muda huo kujifunza zaidi.
  18. Soma kwa dakika 30 kila siku. Huwezi kupiga hatua kama husomi na kujifunza, hivyo kila siku tenga angalau dakika 30 ambazo utazitumia kusoma. Na linda muda huo usiupoteze kwa kingine chochote. Hata kama una mengi kiasi gani, usikose kutenga muda wa kujisomea, ni muhimu sana kwa ukuaji wako.
  19. Jifunze ujuzi mpya unaoweza kuutumia kuikuza biashara yako zaidi. Pamoja na kusoma kila siku, unahitaji kujifunza na kuongeza ujuzi ambao utaweza kuutumia kupiga hatua zaidi kibiashara. Biashara zinabadilika kila siku, ushindani unazidi kuwa mkali, unapaswa kuwa na ujuzi wa ziada ambao utakuwezesha kupiga hatua zaidi.
  20. Kamata mawazo bora yanayokujia kwenye siku yako kwa kuyaandika chini kabla hujayasahau. Unaweza kufanya hivi kwa kuwa na kijitabu kidogo na kuandika, au pia unaweza kutumia simu yako kuandika mawazo unayokutana nayo. Usikubali wazo lolote linalokujia likupotee.
  21. Tengeneza na kuza mtandao wako. Huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe, unahitaji msaada wa wengine ili kuweza kufanikiwa. Hivyo unahitaji kutengeneza na kukuza mtandao wako wa kibiashara. Utengeneze mahusiano bora na wafanyabiashara ambao wanapiga hatua zaidi ambao watakusukuma na wewe upige hatua zaidi.
  22. Timiza ahadi unazotoa. Njia rahisi ya kuwapoteza wateja kwenye biashara ni kuwaahidi vitu halafu usivitekeleze. Jijengee sifa nzuri kwenye biashara yako kwa kuwa mtekelezaji wa kila unachoahidi, kwa kufanya hivyo wateja wanakutegemea na kukuamini.
  23. Tumia nguvu ya HAPANA. Kinachowafanya wengi kushindwa kutimiza ahadi wanazotoa ni kusema NDIYO haraka bila ya kufikiri kwa kina. Kadiri unavyokubali mambo mengi, ndivyo unavyotawanya muda na nguvu zako na ufanisi wako unashuka. Jifunze kusema HAPANA ili kuweka mkazo kwenye yale maeneo muhimu ya biashara yako. Kama kitu siyo muhimu sema HAPANA, na usione aibu waka kuogopa.
  24. Kuwa kiongozi na siyo meneja. Unapowaajiri watu wakusaidie kazi kwenye biashara yako, kuwa kiongozi kwa kuwahamasisha kuchukua hatua na kuwapa uhuru wa kuweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yao. Usiwe meneja ambaye kila kitu kwenye uchukuaji hatua unakisimamia wewe na mtu hawezi kufanya kitu mpaka wewe umwelekeze kwanza. Hilo litakuchosha sana.
  25. Jifunze kuongea. Mtu anayeweza kuongea kwa kujiamini kuhusu kile anachouza anaaminika zaidi na wateja. Na asiyeweza kuongea vizuri, hata kama anauza kitu kizuri, wateja hawatamwamini sana. Jifunze jinsi ya kuongea vizuri, kwa ushawishi na ubobezi na utawafanya watu waamini kwenye kile unachowaelezea.
  26. Jifunze kusikiliza. Kuongea tu hakutakusaidia sana kama hutakuwa msikilizaji, jifunze kusikiliza pale wengine wanapoongea. Na siyo unasikiliza tu kwa masikio, bali pia unaangalia lugha za vitendo ambazo mwongeaji anakuwa anatumia, hivi ni viashiria ambavyo vitakueleza mengi zaidi.
  27. Fanya mazoezi mara kwa mara. Mazoezi ya viungo yana manufaa makubwa sana kwako kiafya na kiufanisi kwenye majukumu yako, hivyo tenga muda wa kufanya mazoezi kila siku. Ukiweza kupata dakika 30 za mazoezi kila siku, utapunguza hatari ya magonjwa kama kisukari na presha, na pia utaongeza ufanisi wako kwenye kazi zako. Pia tafiti zinaonesha watu wanaofanya mazoezi wana kipato kikubwa kuliko watu wasiofanya mazoezi. Hebu anza kufanya mazoezi kila siku na utashangaa jinsi kipato chako kitakavyoanza kuongezeka.
  28. Ishi maisha bora kiafya. Mazoezi ni hatua moja ya kuwa na afya bora. Hatua nyingine ni ulaji na kujikinga na hatari za magonjwa. Kula kiafya, epuka vyakula vya haraka, epuka vilevi, sigara, madawa ya kulevya na jiepushe na vihatarishi vya magonjwa. Afya yako ni mtaji muhimu sana kwako, isipokuwa imara hutaweza kufanya chochote kikubwa.
  29. Pata usingizi wa kutosha. Wajasiriamali wengi hujisifia kwa jinsi wanavyoweza kulala kidogo na kufanya kazi masaa mengi. Usiingie kwenye mtego huo, hakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala, kulingana na uhitaji wa mwili wako. Miili yetu inatofautiana, kwa wastani masaa nane yanashauriwa kiafya, lakini wapo wanaohitaji machache zaidi ya hayo na wapo wanaohitaji mengi zaidi. Hivyo jua uhitaji wa mwili wako, kama masaa nane ndiyo yanakutosha basi pata masaa nane. Kama masaa 6 au 7 yanakutosha pata muda huo wa kulala. Kitu muhimu zaidi kupima kwako siyo masaa mangapi hujalala, bali umezalisha nini kwenye muda wako. Kadiri unavyopumzika zaidi, ndivyo unavyoweza kuzalisha zaidi.
  30. Fanya tahajudi au kuandika jarida lako kila siku. Tahajudi ni zoezi ambalo huwa linafanywa na karibu dini na falsafa zote. Kila dini au falsafa watu wana utaratibu wao wa kutuliza fikra zao na kutafakari yale muhimu. Pia unaweza kuandaa zoezi lako la tahajudi kwa kutafakari yale muhimu zaidi kwako. Pia unaweza kufanya zoezi la kuandika jarida lako kila siku, kila siku unakaa chini na kuandika mawazo yako kwenye kijitabu chako, kwa njia hii unapata utulivu wa kipekee kwako.
  31. Fanya kile unachopenda kufanya. Pamoja na kuwa kwenye biashara, unapaswa kutenga muda wa kufanya kile unachopenda kufanya, ambacho hakihusiani na biashara yako. Hupaswi kuwa mtu wa kufanya na kufikiria kazi muda wote. Tenga muda wa mapumziko ambao utautumia kufanya vile vitu unavyopenda kufanya, ambavyo havihusiani na kazi au biashara yako.
  32. Wasaidie wengine. Ni rahisi kukazana na malengo ambayo umejiwekea na kuona huna muda wa kuwasaidia wengine. Lakini njia rahisi ya kupata chochote unachotaka ni kuwasaidia wengine kupata kile wanachotaka. Mara kwa mara jitolee kufanya kazi za kijamii, wasaidie wanaoweza na hata biashara yako iwe ina lengo la kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na siyo tu kupata faida.
  33. Kadiri unavyokuwa kwenye ujasiriamali, ndivyo hali ya wasiwasi inavyojijenga ndani yako. Unapata hali fulani ya hofu kwamba huenda mafanikio unayopata ni bahati tu na ipo siku mambo yatabadilika na kila mtu atagundua kwamba hukuwa na mafanikio halisi bali bahati tu. Jua hali hii humpata kila anayepiga hatua za mafanikio, na njia pekee ya kuishinda ni kujiamini wewe mwenyewe. Hata kama kuna bahati umekutana nayo, amini juhudi na maandalizi uliyoweka yamekusaidia. Na pia jua hata kama utapoteza kila ulichonacho, utaweza kuanza tena na kufanikiwa.

Rafiki, hizi ndizo tabia 33 ambazo wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wanaziishi kila siku. Anza kuzijenga tabia hizi ndani yako na kuziishi kila siku ili na wewe uweze kufanikiwa zaidi.

Na kwa kumalizia, waandishi wanatushirikisha hatua tisa za kujenga tabia mpya na kuiwezesha tabia hiyo kuwa sehemu ya maisha yako.

Kwa kifupi sana nikushirikishe hatua hizi;

Moja; jenga tabia moja kwa wakati.

Mbili; unaweza kuunganisha tabia zinazoendana na kuzijenga kwa pamoja.

Tatu; fanyia kazi tabia hiyo mpya kwa siku 30 bila ya kuacha hata siku moja.

Nne; unganisha tabia mpya unayojenga kwenye tabia ya zamani uliyonayo.

Tano; chukua hatua ndogo kwenye tabia mpya unayojenga.

Sita; jijengee uwajibikaji kwenye tabia mpya unayojenga, uwe na mtu wa kukusimamia.

Saba; vuka vikwazo kwa kuwa na mpango mbadala.

Nane; jipongeze kwa kila hatua unayopiga.

Tisa; jijengee utambulisho mpya, kwa kujitambulisha kama mtu mwenye tabia ile unayoijenga.

Rafiki, sasa ushindwe tu wewe mwenyewe kwenye kujijengea tabia za mafanikio kwenye maisha yako. Tabia umeshazijua na njia ya kuzijenga tayari unayo, kilichobaki ni wewe kuchukua hatua. Kila la kheri.

#2 MAKALA YA JUMA;  IMANI 10 POTOFU ZINAZOKUZUIA USIWE TAJIRI.

Rafiki, juma hili nilikushirikisha makala kuhusu imani potofu kumi ambazo zinawazuia wengi kufikia utajiri. Imani hizi zimekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku kiasi kwamba hatujui kama ni kikwazo kwetu.

Kama hukusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa ili ujue imani hizo na kuziepuka; Imani Saba (7) Potofu Zinazokuzuia Usiwe Tajiri Kwenye Maisha Yako Na Jinsi Ya Kuzivuka.

Pia nilikushirikisha makala ya hatua za kuchukua mwezi disemba ili mwezi januari uwe bora kwako, unaweza kuzijua hatua hizo hapa; Mambo Kumi (10) Ya Kufanya Mwezi Disemba Ili Mwezi Januari Uwe Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

#3 TUONGEE PESA; KANUNI KUU YA KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA.

Rafiki, kwa kuwa tunaelekea kuumaliza mwaka na kuanza mwaka mwingine, ninapenda tukumbushane kanuni kuu ya kuelekea kwenye utajiri na uhuru wa kifedha.

Ipo kanuni moja kuu, kanuni ambayo wote waliotajirika wameitumia, kanuni ambayo hata wewe ukiitumia utaweza kutajirika sana.

Nataka uikumbuke kanuni hii muda wote wa maisha yako, yaani ikae kwenye kila seli ya ubongo wako.

Kanuni hii ni JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA.

Kwenye kila kipato unachoingiza, kabla hujafanya matumizi yoyote, chukua sehemu ya kipato hicho na weka pembeni. Fedha hiyo unakuwa umejilipa wewe na hupaswi kuiweka kwenye mahesabu yoyote. Unapaswa kuiweka kwenye akaunti maalumu na baadaye unaitumia kuwekeza zaidi.

Maswali muhimu;

Swali; Je ni kiasi gani cha kipato changu niweke pembeni?

Jibu; Kwa kuanza anza na kiwango ambacho hakitakuumiza, lakini endelea kuongeza kadiri unavyokwenda. Asilimia kumi ni kiasi kizuri, lakini unaweza kuanzia chini ya hapo na ukaenda zaidi ya hapo. Muhimu ni ujilipe na maisha yako yaweze kuendelea pia.

Swali; kwa nini unasema nijilipe wakati fedha yote ni yangu?

Jibu; (kicheko), usijidanganye tena hivyo siku nyingine, fedha unayopokea siyo yako, kwa sababu baada ya muda mfupi unamlipa kila mtu, unamlipa anayekuuzia vyakula, anayekuuzia nguo, unalipia umeme, maji, nyumba, gari, mafuta na kila kitu. Halafu unajidanganya ni fedha yako? kabla hujaanza kutumia fedha, weka pembeni kile unachojilipa na usikitumie kwa namna yoyote ile.

Swali; mimi huwa naweka akiba kwa ajili ya dharura na mipango yangu ya baadaye, je hapo si nimejilipa?

Jibu; akiba na kujilipa ni vitu viwili tofauti kabisa, akiba unapaswa kuwa nayo. Na ile fedha unayojilipa haipaswi kuwa na mipango mingine yoyote kwa matumizi au maendeleo. Hii ni fedha ambayo utaiwekeza sehemu ambayo itazalisha zaidi bila ya wewe kufanya kazi.

Swali; je ni sehemu gani ninazoweza kuwekeza kwa mimi ambaye najilipa kidogo kidogo.

Jibu; zipo sehemu nyingi za kuwekeza kama unajilipa kidogo kidogo. Unaweza kuwekeza kwenye mifuko ya vipande vya UTT, unaweza kuwekeza kwa kununua hisa. Na pia unaweza kuwekeza kwenye ardhi na majengo kulingana na kiasi unachojilipa na unavyoweza kukikusanya.

Rafiki, jilipe wewe mwenyewe kwanza na ile fedha unayojilipa usiiweke kwenye mipango mingine yoyote bali uwekezaji ambao utakulipa zaidi baadaye.

Hii ndiyo njia pekee ya kuifanya fedha ikufanyie kazi, badala ya wewe kuifanyia kazi siku zote.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; SEMINA YA TABIA ZA KITAJIRI.

Rafiki, nimekuandalia semina ya kuuanza mwaka 2019 kwa utofauti mkubwa sana, utakwenda kuuanza mwaka 2019 kwa lengo kubwa la kufikia utajiri. utakwenda kujifunza tabia kumi ambazo matajiri wote wakubwa wanazo, ambazo hata wewe unaweza kuwa nazo na zikakusaidia sana.

Nimekuandalia semina ya TABIA ZA KITAJIRI, semina ambayo itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo utaweza kushiriki ukiwa popote duniani.

Semina hii itaanza tarehe 03/01/2019 mpaka tarehe 13/01/2019.

Ili kushiriki semina hii unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA au kama siyo mwanachama basi ulipe ada ya tsh elfu 20 (20,000/=).

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253.

Mwisho wa kulipia ni tarehe 02/01/2019 ila nafasi zikijaa kabla hutapata tena nafasi.

Unaweza kumlipia mtu wa karibu kwako akajifunza.

Kujiunga na kundi la semina hii tumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv  (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).

Karibu sana tupate maarifa sahihi ya kutujenge tabia zitakazotufikisha kwenye utajiri mkubwa.

#5 KAULI YA KUFIKIRISHA; UNAFANIKIWA KWANZA KABLA YA KUPATA FEDHA.

‘Successful people make money. It’s not that people who make money become successful, but that successful people attract money. They bring success to what they do.’ – Wayne Dyer

Watu walifanikiwa wanatengeneza fedha. Siyo kwamba watu wanaotengeneza fedha ndiyo wanaofanikia, bali wanaofanikiwa ndiyo wanaovutia fedha. Wanapeleka mafanikio kwenye kile wanachofanya.

Rafiki, hii ni kauli muhimu sana ya kutafakari kwa sababu tumekuwa tunakosea mara zote, tukifikiri kwamba ukipata fedha ndiyo unafanikiwa. Kumbe ukweli ni kwamba ukifanikiwa ndiyo unapata fedha.

Kwa maneno mengine, fedha haitangulii mafanikio, bali mafanikio yanatangulia fedha. Unapoona mtu ana fedha, alianza kwanza kufanikiwa ndiyo akavutia fedha.

Hivyo kazana kufanikiwa kwenye chochote unachofanya na utaanza kuzivuta fedha kuja kwako.

Rafiki, naamini juma hili la 50 linaisha vizuri sana kwako, kinaisha ukiwa na maarifa mapya pamoja na hamasa ya hali ya juu sana ya kwenda kufanya makubwa zaidi kwenye juma la 51 tunalokwenda kuanza.

Neno langu kwako ni moja tu, FANYA. WACHA MANENO, WEKA KAZI.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu