“Respect yourself enough to walk away from anything that no longer serves you, grows you or makes you happy.” – Grant Cardone
Ni bahati iliyoje kwa sisi kupata nafasi ya kipekee ya kuiona siku hii ya leo.
Siyo kwamba sisi ni wajanja kuliko wengine mpaka tukaweza kuiona siku hii, bali ni bahati ambayo tumeipata.
Na njia bora ya kulipa bahati hii ni kutumia vizuri muda huu tulionao leo, kwa kufanya yale muhimu na kutokupoteza muda kabisa.
Twende tukaiishi siku hii ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA na tutaweza kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari THUBUTU KUACHA NA KUONDOKA…
Huwa tunaanza vitu kwenye maisha yetu tukiwa na nia bora kabisa.
Tukijua vitu hivyi vitatuwezesha kufika kule tunakotaka kufika.
Inaweza kuwa ni kazi, biashara, masomo na hata mahusiano.
Lakini baada ya kuanza vitu hivyo, tunagundua ya kwamba siyo kama tulivyodhania.
Baada ga kuingia ndani tunakutana na uhalisia ambao ni tofauti kabisa na matarajio yetu.
Kile tunachopata kinakuwa hakina mchango wa kutufikisha kule tunakotaka kufika.
Na hapa ndipo shida kubwa inapoanzia,
Kwa kuwa mtu unakuwa umeshaanza kitu hicho, inakuwa vigumu sana kwako kukiacha.
Kwa kuwa unakuwa umeshaweka nguvu, muda na wakati mwingine fedha, unaona huwezi kupoteza vyote hivyo.
Hivyo unaendelea kukomaa, na kuendelea kwako kunakufanya upoteze mudanna nguvu zaidi.
Rafiki, unapaswa kujiheshimu kiasi cha kutosha, kuweza kuthubutu kuacha na kuondoka kwenye kitu chochote ambacho hakina mchango kwenye mafanikio yako makubwa.
Haijalishi umewekeza nini, kama kitu hakikufikishi kule unakotaka kufika, hakikuwezeshi kukua na hakikupi furaha kifanya, unapaswa kuachana nacho, mara moja.
Ni kweli kwa kuacha utaumia wewe na hata kuwaumiza wengine pia. Lakini bora kuumia kidogo sasa kuliko maumivu makubwa baadaye.
Kama unapanga kusafiri kutoka dar kwenda mtwara ila kwa kutokujua ukakata tiketi kwenye gari linaloenda moshi, safari inapoanza unagundua gari haiendi uelekeo wa mtwara, kung’ang’ana kwenye basi hilo kwa sababu tu umeshatoa nauli hakutakusaidia. Na kadiri unavyochelewa kufanya maamuzi ya kushuka, ndivyo unavyozidi kupotea kwenda mbali zaidi na itakugharimu zaidi kurudi sehemu sahihi.
Tafakari leo kwenye kila unachofanya, kwenye kila mahusiano uliyonayo, je vitu hivyo vina sifa hizi tatu?
👉🏼kukuhudumia au wewe kutoa huduma kwa wengine.
👉🏼kukuwezesha kukua zaidi.
👉🏼kukupa furaha unapofanya.
Kama vitu hivi vitatu havipo, ni wakati sasa wa kutumia uthubutu wako kufanya maamuzi ya kuacha na kuondoka.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuthubutu kuacha na kuondoka kwenye yale ambayo hayana mchango tena kwenye maisha yako.
#ThubutuKuacha, #Using’ang’aneKupotea, #HudumaUkuajiNaFuraha
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha