Kupata wazo jipya siyo kazi, mawazo mapya yapo mengi mno. Hakuna aliyeshindwa kwenye maisha kwa sababu hakupata wazo jipya na zuri.

Watu wengi wanashindwa kwenye maisha kwa sababu wanashindwa kusahau wazo la zamani, wanashindwa kuachana na wazo walilokuwa wanafanyia kazi siku za nyuma.

Huwa tunapenda sana vitu vyetu, na tunaendelea kuvipenda hata pale ambapo havina matumizi kwetu. Wakati mwingine tunaving’ang’ania kwa sababu hatuna uhakika kama vipya tunavyopata vitakuwa bora.

Na wakati mwingine tunaving’ang’ania kwa sababu tu tumeshazoea, tumeshaviona ni sehemu ya maisha yetu na kuachana navyo itakuwa kama tunayaharibu maisha yetu.

Moja ya hatua unayopaswa kupiga ili kufanikiwa ni kuwa tayari kuacha na vitu ulivyozoea, kuacha vitu ambavyo hapo nyuma vilifanya kazi vizuri ila kwa sasa unahitaji vingine ili kupiga hatua zaidi.

Mwandishi mmoja amewahi kuandika kitabu chenye jina kilichokufikisha hapa siyo kitakachokufikisha mbele zaidi. Na yupo sahihi sana, ulichofanya jana ukapata matokeo ya leo, ukikifanya leo unaweza usipate matokeo mazuri kesho kama uliyopata leo.

Tunapaswa kupunguza mapenzi na mawazo yetu ya nyuma, ambayo kwa sasa hayafanyi kazi tena, au njia tulizozoea ambazo kwa sasa hazileti matokeo bora kama zamani.

Na ni lazima uwe tayari kwa maumivu, ili kutengeneza kitu kipya, cha zamani lazima kiharibiwe. Yai ni zuri sana, lina mwonekano mzuri na virutubisho vizuri ndani yake. Lakini ili liwe kuku, lazima kwanza liharibike kama yai, lazima lipasuliwe ndiyo maisha ya kuku yaanze. Kama yai litataka kubaki kama yao, halitaweza kuwa kuku na kuzalisha mayai zaidi.

Kuwa tayari kwa wakati wowote kupoteza kile ulichozoea ili kuweza kupata kile ambacho ni bora zaidi ya ulichonacho sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha