Hakuna mtu anayejua kila kitu, na hii ni habari njema kwa sababu kila mtu anayo nafasi ya kujifunza zaidi.
Pia hakuna mtu ambaye hakuna anachojua kabisa, na hii pia ni habari njema kwa sababu kila mtu ana kitu anachoweza kuwafundisha wengine.
Kujua na kutokujua ni hali mbili ambazo kila binadamu anazo, na hivyo tunapaswa kuzitumia hali hizi mbili vizuri kwa ajili yetu na hata wale wanaotuzunguka.
Wengi huwa hawapendi kukubali kwamba hawajui, hivyo wanakuwa hawapo tayari kujifunza, kitu ambacho kinawazuia wasijue kile ambacho hawajui. Usikubali kuwa kwenye kundi hili la wale wasiojua lakini wanataka waonekane wanajua. Hakuna ubaya wowote kwenye kutokujua, bali kuna uzuri kwa sababu unapata nafasi ya kujua.
Kwa wale ambao wanajua, wamekuwa hawajiamini kwa kile wanachojua. Wengi huona ni kitu kidogo au cha kawaida sana kiasi kwamba hawawezi kumfundisha mtu mwingine yeyote. Usiingie kwenye kundi hili pia, kwa sababu utawanyima wengine fursa na hata wewe mwenyewe utajinyima fursa. Kwa kuwafundisha wengine kile unachojua, kunakupa nafasi ya kukijua kwa undani zaidi. Pia unapowafundisha wengine, wananufaika na kile unachojua wewe.
Tumia kujua na kutokujua kwako kama njia ya wewe na wengine kujua zaidi. Usione aibu kwamba hujui na wala usiwe na hofu kwamba unachojua hakina msaada. Kujua na kutokujua ni hali ya kawaida kwa kila mmoja wetu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana mungu akubariki tuzidi kupata maarifa haya muhimu
LikeLike
Karibu
LikeLike