Yupo huru mtu yule awezaye kusema chochote anachotaka kusema, bila ya kujali wengine wanasemaje au kuchukuliaje. Uhuru ni ngazi ya kwanza kabisa katika kujitambua kama mtu na kuweza kupiga hatua kubwa,

Jasiri ni yule ambaye anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya na anachoamini ni muhimu kufanya, bila ya kujali wengine wanaamini na kufanya nini. Kufanya unachotaka kunahitaji ujasiri mkubwa kwa sababu wengi wanataka ufanye kile wanachofanya wao.

Bora ni yule ambaye anaweza kusikiliza kila aina ya maoni, kujifunza na kisha kutengeneza maoni yake mwenyewe. Yule ambaye halazimiki kubeba maoni ya wengine kwa sababu tu ndivyo wengi wanavyofikiria. Ni watu hawa bora ndiyo wanaowasaidia wengine kupata uhuru wao.

Dhana hizo tatu ni rahisi sana kuzitamka kuliko kuzitekeleza kwenye maisha, wengi huzungumzia uhuru kama kitu rahisi, lakini inapokuja kwenye kusema kile wanachoamini wanashindwa.

Wengi hutamani kuwa jasiri, lakini inapokuja kwenye matendo ya kudhihirisha ujasiri wao wanashindwa kuyatekeleza.

Na wengi hutamani kuwa bora na kuwa na maono yao, lakini maoni ya wengi yanawateka na kujikuta wapo ndani ya kundi.

Sema kile unachotaka kusema, ambacho unajua ni sahihi, fanya kile unachotaka kufanya ambacho unaamini ni sahihi na simama kwa miguu yako mwenyewe, kwa kuwa na maoni yako mwenyewe. Hivyo ndivyo unavyokuwa mtu bora na wa mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha