Watu wengi huwa hawapendi kujiwekea viwango vyao vya utendaji, kwa sababu wanaona wakishindwa kuvifikia basi watakuwa wamefeli kwenye maisha yao.
Ni kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa hawapendi kuweka malengo kwa sababu wasipoyafikia basi watajiikia vibaya.
Faida ya kujiwekea viwango vyako vya utendaji kwenye maisha siyo kufikia viwango hivyo, bali kuwa na njia ya kujipima.
Unapokuwa na viwango vyako vya utendaji, ni rahisi kujua kama umefanya vizuri au vibaya. Kwa sababu utakuwa na kitu cha kujipima na kujilinganisha nacho.
Na hata pale ambapo hufikii viwango hivyo, ni rahisi kusimama na kuanza tena, huku ukiweka juhudi zaidi ili upate matokeo ya tofauti na uliyopata mwanzo.
Kama huna viwango, utaendelea kurudia yale yale na kupata matokeo yale yale.
Kama huna viwango vyako unavyofanyia kazi ni rahisi kujidanganya wewe mwenyewe na hata kusikia uongo wa wengine kwamba upo vizuri. Haupo vizuri kwa kujifikiria au kwa sababu wengine wamekuambia hivyo. Unakuwa vizuri pale unapofanya kulingana na viwango vyako.
Jiwekee viwango vyako vya utendaji leo, viwango hivyo viwe vya juu sana, ambavyo vitakusukuma ufanye zaidi ya ulivyozoea kufanya. Viwango hivyo vitakuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,