Hivi ni vitu viwili ambavyo lazima uvifanye kila siku, hata kama hujisikii kufanya, hata kama huna muda wa kuvifanya, utatenga muda na kuvifanya. Kila siku.

Lakini inapokuja kwenye mambo mengine muhimu sana ambayo tunapaswa kuyafanya kila siku, tunaanza kujipa sababu kwa nini hatuwezi kufanya kila siku.

Chukulia kitu muhimu kama kujifunza na kujiendeleza zaidi. Hiki ni kitu ambacho unapaswa kukifanya kila siku, lakini wengi hutafuta sababu kwa nini wasifanye kila siku.

Na haishangazi kuona wengi wamekwama kwenye maisha yao, hawapigi tena hatua kufanikiwa zaidi.

Wapo watu ambao hawajawahi kusoma kitabu chochote au kujifunza kitu kipya kuhusiana na kazi au biashara wanayofanya. Wanafanya tu kwa mazoea kitu ambacho kinakuwa kikwazo kikubwa kwao.

Wapo wengine ambao wanafikiri wakisoma kitabu kimoja, wakihudhuria semina moja au kupata mafunzo fulani mara moja basi inatosha kabisa kuwafikisha kwenye mafanikio makubwa kwa maisha yao yote.

Kote huku ni kujidanganya na kutetea pamoja na kuficha uvivu ambao upo ndani ya mtu.

Kitabu kimoja, semina moja au mafunzo fulani ya aina moja hayatakufikisha popote kwenye maisha yako. Kama ilivyo kwamba kula mara moja au kuoga mara moja haimaanishi ndiyo unashiba kwa maisha yako yote.

Hivyo weka kipaumbele cha kujifunza kila siku kwenye maisha yako, tenga kabia muda ambao utakuwa ni wa kujifunza. Ondokana na kila aina ya kelele na kaa chini kwa muda uliopanga na ujifunze. Kwa wewe ambaye upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, isiwe chini ya masaa mawili kwa siku.

Kaa chini kwa utulivu na ujifunze kwa kina, na ukishajifunza chukua hatua siku hiyo hiyo kwa kuanza kutumia kile ambacho umejifunza. Kwa sababu ukisema usubiri mpaka utakapokuwa tayari, utasahau na ule moto uliowasha ndani yako utapoa.

Kujifunza na kupiga hatua zaidi ni zoezi la kufanya kila siku, tuache kulifanya kwa kujisikia au kusema mpaka tutakapopata muda. Ni lazima utenge muda na kuutumia kwa kusudi hilo kama unachotaka ni kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Hata ubanwe kiasi gani, lazima utenge muda wa kula, basi fanya hivyo kwenye kujifunza pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha