#TANO ZA JUMA #4 2019; Kwa Nini Saba, Tabia Za Mafanikio Za Mamilionea, Vitabu 117 Vilivyosomwa Mwaka 2018, Furaha Zao La Fedha Na Furahia Magumu Unayopitia.

Rafiki yangu mpendwa,

Ni juma la nne la mwaka huu 2019 linakwenda kutuacha, mwaka ambao majuzi tulisema ni mpya, kwa sasa unazidi kumaliza upya wake.

Matumaini yangu ni kwamba upya uliouanzisha ndani yako bado unaendelea, malengo makubwa uliyojiwekea bado unayafanyia kazi na hamasa kubwa uliyoanza nayo mwaka huu bado unaendelea kuichochea.

Hilo ndilo pekee ambalo unahitaji ili uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, kwa sababu wengi hupanga, wengi huanza lakini wanaoendelea na hata kufikia kwenye kilele ni wachache mno. Wakianza 100, mmoja ndiye anayefika kwenye kilele cha mafanikio, wengine wanaishia njiani. Matumaini yangu ni kwamba mmoja anayefika kwenye kilele ni wewe. Na ndiyo maana tupo pamoja hapa, tukipeana maarifa sahihi ya kufika kwenye kilele cha mafanikio.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi ili maisha yako yaweze kuwa bora na ufike kwenye kilele cha mafanikio.

Soma tano hizi za juma, zitafakari kwa kina na panga ni hatua zipi unazokwenda kuchukua kwenye maisha yako ili uweze kufika kwenye kilelecha mafanikio yako.

Karibu.

#1 NENO LA JUMA; KWA NINI SABA.

Mara nyingi tumekuwa tunafanya vitu bila ya kujua kwa nini hasa tunafanya. Tunaweza kufikiri tunajua kwa nini tunafanya, ila kwa nini tunayokuwa nayo inakuwa ni ya juu juu sana, siyo ile kwa nini ya ndani kabisa.

Sasa madhara ya kutokujua kwa nini ya ndani ni kuishia njiani, hasa pale unapokutana na magumu, na kila mtu huwa anakutana na magumu kwenye maisha yake.

Pale unapoanza kufanya kitu chochote kipya na kikuba, unakutana na magumu na changamoto ambazo hukujua. Hata kama ulijiandaa kiasi gani, bado kuna ugumu utakaokutana nao.

Kitu pekee kitakachoweza kukuvusha kwenye ugumu wowote unaokutana nao ni ile KWA NINI ya ndani, kwa nini halisi inayokusukuma kupata unachotafuta.

Ili kujua KWA NINI YA NDANI ya chochote unachofanya, unapaswa kujiuliza maswali saba muhimu ambayo yatakufikisha kwenye sababu hiyo halisi ya unachofanya.

Maswali hayo saba yote ni ya kwa nini.

Kwa mfano kama lengo lako ni kuwa bilionea,

Swali la kwanza ni kwa nini unataka kuwa bilionea? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka uhuru wa kifedha.

Swali la pili ni kwa nini unataka kuwa na uhuru wa kifedha? Jibu linaweza kuwa kwa sababu umepitia maisha magumu na hutaki kurudi tena kwenye aina hiyo ya maisha.

Swali la tatu ni kwa nini hutaki kurudi kwenye maisha magumu? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka kuwa huru na maisha yako, hutaki ukosefu wa fedha uwe kikomo kwako.

Swali la nne ni kwa nini unataka kuwa na uhuru na maisha yako? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka uweze kuwasaidia wengine wenye uhitaji.

Swali la tano ni kwa nini unataka kuwasaidia wengine wenye uhitaji? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka kuacha sifa nzuri kwako na kwa familia yako.

Swali la sita ni kwa nini unataka kuacha sifa nzuri kwako na kwa familia yako? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka kuwa na mchango na kuacha alama hapa duniani.

Swali la saba ni kwa nini unataka kuacha alama hapa duniani? Jibu linaweza kuwa kwa sababu unataka kuwa na udhibiti wa maisha yako na kuwawezesha wengine kuwa na udhibiti wa maisha yao.

Kwa mfano huu, unaona jinsi ambavyo sababu ya ndani, ile KWA NINI halisi ilivyo na nguvu kubwa na inavyoweza kukusukuma zaidi.

Kwa kila unachopanga kufanya, tenga muda na ufanye zoezi hili la KWA NINI SABA na utaweza kupata sababu halisi itakayokusukuma hata pale unapokutana na ugumu kwenye safari yako ya mafanikio.

#2 KITABU CHA JUMA; TABIA ZA MAFANIKIO ZA MAMILIONEA.

Rafiki yangu mpendwa, juma hili la nne nimesoma kitabu cha TABIA ZA MAFANIKIO ZA MAMILIONEA. Kitabu kinaitwa MILLIONAIRE SUCCESS HABITS: The Gateway To Wealth & Prosperity ambacho kimeandikwa na Milionea Dean Graziosi.

millionaire success habits

Hiki ni kitabu ambacho Dean anatushirikisha tabia ambazo zimeweza kumtoa yeye kwenye masikini wa kutupwa mpaka kwenye utajiri wa ngazi ya umilionea. Tunapozungumzia umilionea ni kwa thamani ya dola za kimarekani, ambapo dola milioni moja ya kimarekani kwa sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 2 na milioni mia tatu.

Dean Graziosi ni nani?

Mwandishi wa kitabu cha MILLIONAIRE SUCCESS HABITS ni bilionea mwekezaji kwenye majengo, mjasiriamali, mwandishi na kocha wa mafanikio.

Dean ametokea kwenye maisha magumu, alitokea familia masikini ambayo wazazi wake walitengana na kujikuta akiishi na wazazi wengi wa kambo kwenye utoto wake.

Pia akiwa mtoto hakuwa anafanya vizuri shuleni, kitu kilichokuja kujulikana baadaye kwamba alikuwa na uwezo mdogo wa kuelewa darasani. Hilo lilimfanya ashindwe kufika elimu ya juu na hivyo kuanza biashara akiwa mdogo.

Kwa kutokea kwenye umasikini mkubwa, huku akiwa hana elimu kubwa, kitu pekee kilichomwezesha kufikia mafanikio makubwa ni kuweka juhudi kwenye kila alichofanya na pia kujifunza kupitia wale waliofanikiwa. Moja ya watu anaowashukuru sana ambao wamemsaidia kufika alipofika kwa mafunzo yao ni Mwandishi na mhamasishaji Tony Robbins.

Pamoja na kuwa milionea kupitia uwekezaji wa majengo, Dean pia ameandika vitabu vingi ambavyo vimeweza kufikia umaarufu mkubwa kwenye chati ya vitabu ya jarida la NEW YORK TIMES.

Vitabu vingine vilivyoandikwa na Dean ni; Totally Fulfilled, Be a Real Estate Millionaire, Thirty Days to Real Estate Cash, Your Town, Your Profits, and Profit from Real Estate Right Now.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu chake cha MILLIONAIRE SUCCESS HABITS ambapo anatushirikisha tabia alizojifunza kwa waliofanikiwa na zilizomwezesha yeye kutoka kwenye umasikini na bila ya elimu kuweza kufika kwenye mafanikio makubwa.

Moja; MUDA NI SAHIHI KUBADILI TABIA ZAKO.

Kitu pekee kinachokuzia wewe usipate yale matokeo ambayo wengine wanayapata, ni tabia ambazo unaziishi sasa. Kama ukijua tabia za waliofanikiwa na ukaziishi, basi utaweza kupata matokeo ambayo wanayapata.

Tofauti kuu kati ya waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa ni kwamba waliofanikiwa wanafanya vitu ambavyo wasiofanikiwa hawataki kuvifanya.

Unaweza kubadili tabia zako sasa na ukaianza safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa. Zijue tabia sahihi na ziishi tabia hizo, utaweza kufanikiwa sana.

Mbili; MSINGI MKUU WA MAFANIKIO YOTE.

Changamoto kubwa ya zama hizi ni kwamba kila mtu anakwenda kasi, lakini cha kushangaza hajui anakwenda wapi. Kila mtu yupo bize kila siku, anaamka asubuhi na mapema na kuchelewa kulala, lakini hajui wapi anayapeleka maisha yake.

Haijalishi unakwenda kiasi gani, kama hujui unakokwenda, kasi uliyonayo inakupoteza tu.

Msingi mkuu wa mafanikio yote ni kujua nini hasa ambacho unakitaka, kuwa na maono ya kile unachotaka kwenye maisha yako. Ukishajua kwa hakika nini unachotaka, hutasongwa tena na mambo ambayo siyo muhimu kwako.

Dean anasema kama kila siku upo bize na huna muda wa kukamilisha mambo yako, ni dalili kwamba hujui unachotaka au hujui unakokwenda.

Anza kwa kujua nini hasa unachotaka, wapi hasa unakotaka kufika, kisha jua hatua zipi muhimu za kuchukua ili kufika unakotaka kufika, kisha puuza mengine yote ambayo hayachangii wewe kufika unakotaka kufika.

TATU; NAFSI MBILI ZILIZOPO NDANI YAKO NA NAFSI YA KUDIDIMIZA.

Kila mmoja wetu ana nafsi mbili zilizopo ndani yake. Nafsi moja ni chanya na inakupa hamasa ya kupiga hatua zaidi. Nafsi nyingine ni hasi na inakukatisha tamaa kwa kuangalia upande mbaya wa kila jambo.

Kudhibitisha uwepo wa nafsi hizi mbili ndani yako, fikiria kipindi ambacho umewahi kupata wazo kubwa ambalo lingeweza kuyabadili maisha yako. Haikuchukua muda wewe mwenyewe ukaanza kujiambia huwezi, ni ngumu, utashindwa na mengine ambayo yalikuzuia kupiga hatua.

Sasa njia ya kukuwezesha wewe kufanikiwa ni kulisha ile nafsi chanya na kuididimiza nafsi hasi. Kulisha nafsi chanya hakuna shida sana, kazi kubwa ipo kwenye kudidimiza ile nafsi hasi.

Dean anatushirikisha mambo yafuatayo yatakayotusaidia kudidimiza ile nafsi hasi iliyopo ndani yetu ili isituzuie kufanikiwa.

 1. Jipe dayati ya habari, usiangalie, kusikiliza wala kufuatilia habari yoyote ile kwa siku 30. Hakuna kitu kinacho chochea nafsi hasi kama habari, maana sehemu kubwa ya habari ni mambo hasi. Achana na habari na nafsi hasi iliyopo ndani yako itadidimia.
 2. Fanyia kazi yale maeneo ambayo una uimara na achana na madhaifu yako. Tumekuwa tunaambiwa tufanyie kazi madhaifu yetu, lakini huko ni kuyafanya yawe imara zaidi. Fanyia kazi uimara wako na achana kabisa na madhaifu yako.
 3. Puuza ushauri mbaya kutoka kwa watu wasiokuwa na sifa ya kutoa ushauri wanaotoa. Ndugu, jamaa na marafiki wanaweza kuona wana ushauri mzuri sana kwako kuhusu mafanikio, lakini wao wenyewe hakuna mafanikio makubwa waliyopata, na sehemu kubwa ya ushauri wao huwa ni kukatisha tamaa, upuuze kabisa, usichukue hata sehemu ndogo ya ushauri wa aina hiyo.
 4. Usifanye kile ambacho kila mtu anafanya, kwa sababu tu na wewe unabidi ufanye. Fanya kile ambacho ni muhimu kwako kufika unakotaka kufika.
 5. Jichukulie kama mshindi, tabasamu, simama wima na tembea na ongea na wengine kwa kujiamini. Kadiri unavyokuwa katika hali ya kujiamini ndivyo nafsi hasi ya ndani yako inavyodidimia.
 6. Zungukwa na watu wanaokuhamasisha na kukusukuma kupiga hatua zaidi, waepuke wale wanaokuvuta na kukurudisha nyuma.

Nne; TENGENEZA HADITHI YENYE NGUVU KWAKO.

Kila mmoja wetu kuna hadithi ambayo anaiishi, hadithi ambayo umekuwa unajiambia kila siku na imekuwa kikwazo kwako kupiga hatua. Kwa mfano kama umetokea familia masikini na huna elimu, hadithi yako inaweza kuwa kwamba wewe huwezi kufanikiwa kwa sababu umetoka familia masikini na huna elimu kubwa.

Lakini hadithi hiyo ni uongo, ni kweli unaweza kuwa umetoka familia masikini na huna elimu kubwa, lakini hicho siyo kinachokuzuia kufanikiwa. Wapo wengi waliotoka kwenye umasikini mkubwa kuliko wako na hata hawakupata elimu kabisa lakini wamefanikiwa.

Hivyo badili hadithi inayokuzuia kufanikiwa na tengeneza hadithi mpya ya mafanikio yako ambayo itakusukuma kufanikiwa zaidi. Hadithi yako ya mafanikio iguse yale maeneo ambayo una uimara na uyatumie kama sababu ya wewe kufanikiwa.

Hadithi yako mpya iwe ni kinyume kabisa na ile iliyouwa inakuzuia. Ukishaandika hadithi hii jiambie na kujikumbusha kila siku mpaka iwe sehemu ya fikra zako.

Tano; MWAMSHE SHUJAA ALIYE NDANI YAKO.

Kila mmoja wetu ana shujaa aliye ndani yake. Shujaa huyu ni uwezo mkubwa na wa kipekee ambao mtu anao, uwezo usio na ukomo na ambao hakuna mwingine anao hapa duniani.

Njia ya kumwamsha shujaa aliye ndani yako ni kujijengea kujiamini. Tatizo la wengi ni kutokujiamini, kushindwa kusimamia kile wanachotaka, hasa pale ambapo wengine hawakubaliani nao.

Katika kujijengea kujiamini, zingatia vitu vitatu muhimu; uthubutu wa kufanya kitu kipya, dhamira ya kufanya kitu hicho na kutumia uwezo wa ndani yako kufikia kile unachotaka kufikia.

Watu wengi hawajui kwamba ndani yao wana uwezo mkubwa wa kufanya chochote wanachotaka. Wengi huangalia nje na kukoa msaada. kama utaanza kuangalia ndani yako utapata msaada mkubwa kwako kufika unakotaka kufika.

Sita; LENGO MOJA KUBWA LINALONG’AA.

Watu wengi wamekuwa wanakwama kwa kuwa na malengo mengi ambayo hawayafanyii kazi. Pia wanakuwa na majukumu mengi ya kufanya ambayo hayachangii wao kufika kule wanakotaka kufika.

Dean anatuambia tunapaswa kuwa na malengo machache muhimu au lengo moja kuu ambalo tunafanyia kazi na kupuuza mambo mengine yote ambayo hayatusaidii kwenye lengo hili.

Katika kupata lengo hili, zipo hatua muhimu za kuchukua;

 1. Orodhesha vitu vyote ambavyo unapenda kufanya, ambavyo unaweza kufanya hata kama hakuna anayekulipa.
 2. Orodhesha maeneo yote ambayo uko vizuri, kwa ujuzi, zoefu au kipaji.
 3. Orodhesha majukumu ambayo kwa kuyatekeleza utaweza kupata kipato kikubwa. Yaani kwa yale uliyoorodhesha kwenye A na B, chagua yale ambayo ukiyafanya kipato unachopata kinakuwa kikubwa.
 4. Weka malengo yako ya kifedha uliyonayo, malengo ya mwaka mmoja, miaka mitano na hata kumi ijayo.
 5. Hapa sasa chagua majukumu utakayofanyia kazi, ambayo yanakulipa zaidi na yatakayokufikisha kwenye malengo yako ya kifedha. Na fanya hayo tu, mengine yote achana nayo.
 6. Tengeneza orodha ya majumu ya kutokufanya, kama kitu hakijaingia kwenye sehemu E basi kinaingia kwenye orodha hiyo ya majukumu ambayo hutofanya na usiyafanye.

Saba; MVUTO NA USHAWISHI.

Mvuto na ushawishi ni vitu viwili ambavyo kila anayetaka kufanikiwa na kutengeneza kipato kikubwa anapaswa kuwa navyo. Dean anaita vitu hivi viwili kichocheo cha utajiri, vikikosekana huwezi kufikia mafanikio makubwa na utajiri.

Mvuto na ushawishi ni njia nyingine ya kusema MASOKO NA MAUZO. Kila tunachofanya kwenye maisha ni masoko, na kila kinachotuingizia kipato ni mauzo.

Hivyo tunaweza kusema kazi zetu kubwa kwenye maisha ni mbili, MASOKO NA MAUZO. Tunapaswa kujiweka kwa njia ambayo watu wayajua uwepo wetu, na pia tuweze kuwashawishi watu hao kutupa kile ambacho tunataka watupe.

Katika kuboresha masoko na mauzo kwenye biashara zetu, kazi zetu na hata maisha yetu kwa ujumla, Dean anatushirikisha hatua zifuatazo za kuchukua;

 1. Kuwa muwazi na mwaminifu mara zote. Uaminifu unalipa.
 2. Kuwa wewe na kuwa na hamasa, usijaribu kuingiza kuwa mtu mwingine.
 3. Amini kwenye utele na siyo uhaba, amini kuna wingi wa chochote kwa ajili ya kila mtu.
 4. Wape watu kile wanachotaka na siyo wanachohitaji.
 5. Tumia hadithi, watu wanaelewa na kusukumwa zaidi na hadithi na mifano kuliko maelezo pekee.
 6. Usiwe mwongeaji sana, ukishaeleweka nyamaza.
 7. Kuwa na msukumo wa ndani wa kile unachofanya.
 8. Endelea kutengeneza mahusiano na wale ambao unawauzia au wameshakubaliana na wewe.
 9. Tengeneza mtazamo wa shukrani.
 10. Zingatia zaidi kujenga mahusiano kuliko kipato, fanya kile ambacho kitaboresha mahusiano yako na unayetaka kumuuzia au akubaliane na wewe.

Nane; NGUVU YA FURAHA.

Wengi wamekuwa wanafikiri kwamba wakifanikiwa ndiyo watakuwa na furaha. Lakini ukweli ni kwamba furaha ndiyo inaleta mafanikio.

Dean anatushirikisha hatua muhimu za kuchukua ili kujijengea furaha ambayo itatuwezesha kupata mafanikio makubwa;

 1. Jua nini maana ya furaha kwako, kinachokupa furaha wewe siyo kinachowapa furaha wengine.
 2. Ishi kwenye wakati uliopo saa, siyo wakati uliopita wala wakati ujao.
 3. Acha kufikiria sana kuhusu vitu, hasa vile ambavyo hakuna hatua unazoweza kuchukua.
 4. Angalia upande chanya wa kila jambo, hata kama jambo ni baya kiasi gani, lina upande ambao ni mzuri, angalia huo.
 5. Linda amani na utulivu wako wa ndani, ondokana na hali zote hasi.
 6. Elewa kwamba kuteseka ni kuchagua, chagua kutokuteseka.
 7. Pokea kushindwa kwa mikono miwili na chukua hatua ili kuwa bora zaidi.
 8. Usiwe na kinyongo na yeyote, samehe kila mtu.
 9. Usiweke matarajio makubwa na kutegemea kila kitu kitaenda kama ulivyopanga.
 10. Shukuru kwa kilichopo mbele yako.
 11. Usiridhike na kile ulichozoea, uifanye mambo kwa mazoea.
 12. Kuwa sehemu ya kitu kikubwa, jijenge zaidi kiroho na kiimani.

Tisa; NJIA ZA KUKUWEZESHA KUFIKIA MAFANIKIO HARAKA.

Kuna vitu vidogo vidogo ambavyo unaweza kuvifanya kila siku na vikakusukuma zaidi kwenye kufikia mafanikio makubwa. Dean anatushirikisha vitu hivyo kama ifuatavyo;

 1. Tenga muda wa ubunifu wako, muda ambao utafanya kazi bila ya usumbufu wowote. Tenga angalau masaa mawili kwa siku kama muda wa ubunifu kwako.
 2. Angalia kazi za wengine na shukuru, shukuru kwa namna wengine wanavyojitoa kufanya kazi ili kuboresha maisha yao na ya wengine.
 3. Weka alamu za kukukumbusha kushukuru, angalau mara tatu kwa siku. Na alamu inapoita shukuru kwa mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako.
 4. Weka akiba ya fedha, kadiri unavyokuwa na akiba ya fedha ndivyo unavyojiamini na kuvutia fedha zaidi.
 5. Mara kwa mara jipe kile unachopenda hata kama kina gharama kubwa, ni sehemu ya kujikumbusha kwamba kuna utele. Mfano kuwa na mapumziko ya gharama kubwa.
 6. Wekeza ndani yako mwenyewe, jifunze kila siku, soma vitabu, sikiliza angalia mafunzo mbalimbali.
 7. Tabasamu na mwangalie usoni kila unayekutana naye.
 8. Angalia jema kwenye kila ubaya.
 9. Unapoanguka, inuka haraka na endelea na safari.
 10. Angalia suluhisho na siyo tatizo.
 11. Waulize wenye furaha siri ya furaha waliyonayo.
 12. Kwenye fikra zako jikumbushe maeneo ambayo ukiyakumbuka unakuwa na furaha, na jikumbushe maeneo hayo kila unapokutana na ugumu au huzuni.
 13. Weka kipaumbele kwenye afya yako, ulaji na ufanyaji wa mazoezi.
 14. Acha kuwahukumu wengine, jua kila mtu kuna magumu anapitia.
 15. Wasaidie wengine ambao wanapitia magumu kuliko wewe.
 16. Mara zote fanya kwa ubora wa hali ya juu sana, hata kama ni kitu kidogo kiasi gani.
 17. Zama kwenye fikra chanya na upande chanya wa mambo mara zote.
 18. Ajiri watu wenye akili zaidi yako na wenye vipaji ambavyo wewe huna.
 19. Fanyia kazi kitu kimoja kwa wakati mpaka kinapokamilika ndiyo uende kwenye kitu kingine.

Kumi; SASA NI MUDA WAKO.

Kupitia kitabu hiki, Dean siyo tu ametupa mafunzo ya tabia za mafanikio, bali ametupa kanuni ya kufuata kwenye maisha yetu ili tuweze kufanikiwa.

Baada ya kujua kanuni hii na yale tunayopaswa kufanya, jukumu limebaki kwetu kuchukua hatua ili kuweza kufanikiwa zaidi.

Haya yote uliyojifunza, hayatafanya kazi kwenye maisha yako mpaka pale wewe utakapochukua hatua na kuyafanyia kazi.

Dean anasisitiza wakati wa kuchukua hatua ni sasa, siyo kesho au wezi ujao au mwaka ujao, chukua hatua sasa hivi baada ha kujifunza au hutachukua hatua kabisa.

Imani yangu ni kwamba unakwenda kuchukua hatua ili uweze kuyaboresha maisha yako. Nakutakia kila la kheri kwa kila hatua unayokwenda kuchukua na kumbuka mimi Kocha wako niko kwa ajili yako. Unapokwama au kuhitaji mwongozo zaidi usisite kunitafuta, nimejitoa kwa ajili ya mafanikio yako.

#3 MAKALA YA JUMA; VITABU 117 VILIVYOSOMWA MWAKA 2018.

Rafiki, kwenye KISIMA CHA MAARIFA, programu ya mafunzo na ukocha ninayoendesha kupitia kundi la wasap na blog ya KISIMA CHA MAARIFA, wanachama wanapaswa kutimiza baadhi ya vigezo ili kuendelea kunufaika na programu hiyo.

Pamoja na kulipa ada ya mwaka, ambayo kwa sasa ni tsh laki moja, kila mwanachama anapaswa kuwa na njia mbadala za kuingiza kipato, kuweka akiba kwenye kila kipato chake, kuwekeza na pia kujifunza kupitia usomaji wa vitabu.

Kwa muda ambao programu hii ya KISIMA CHA MAARIFA imekuwepo, naweza kusema imeweza kuleta mafanikio makubwa sana kwa wengi ambao wamejiunga na kuwa mwanachama. Hakuna aliyejiunga na KISIMA CHA MAARIFA na akabaki kama alivyokuwa.

Japo wengi huwa na wasiwasi wakati wa kujiunga, wakiona ada ni kubwa, lakini baada ya kujiunga hukiri wenyewe kwamba ada wanayolipa ni ndogo mno ukilinganisha na maarifa wanayoyapata.

Kwa mwaka 2018 tulioumaliza, wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA wameweza kusoma na kushirikisha yale waliyosoma kwenye vitabu vingi sana. katika vitabu hivyo vingi, nimekushirikisha vitabu 117 (mia moja na kumi na saba) pamoja na yale ambayo watu wamejifunza kwa kusoma vitabu hivyo.

Vitabu hivyo pamoja na waliyojifunza yapo kwenye makala hii, ifungue na kusoma kama bado hujaisoma; Vitabu 117 Vilivyosomwa Na Wanachama Wa Kisima Cha Maarifa Mwaka 2018. (https://amkamtanzania.com/2019/01/25/vitabu-117-vilivyosomwa-na-wanachama-wa-kisima-cha-maarifa-mwaka-2018/)

Fungua na usome makala hiyo ili kujua vitabu unavyoweza kuvisoma mwaka huu 2019 kama kuna ambavyo hujasoma. Pia endelea kutembelea www.amkamtanzania.com kila siku kujifunza kwa makala mbalimbali zinazowekwa kila siku ya wiki.

#4 TUONGEE PESA; FURAHA ZAO LA FEDHA.

Ile kauli kwamba matajiri hawana furaha au huwezi kuwa na fedha na ukawa na furaha, ni mtego ambao watu wamekuwa wanajitengenezea wenyewe bila ya kujua.

Ipo hivi rafiki, wengi tunapokuwa tunaanzia chini, huwa tunafikiri tutakapopata fedha basi ndiyo zitakuwa jawabu la kila kitu. Hivyo tunaahirisha maisha yetu yote mpaka pale tutakapopata fedha.

Na hata kwa upande wa furaha, tunaahirisha furaha yetu tukiamini tukishakuwa na fedha basi ndiyo tutakuwa na furaha. Tunaacha kufanya yale mambo madogo madogo ya kila siku ambayo yanatuletea furaha, tukiamini kwamba tukishakuwa na fedha nyingi, basi furaha itakuja yenyewe.

Lakini hilo ni kinyume kabisa na msingi wa furaha, fedha haileti furaha, bali furaha inaleta fedha. Kwa kifupi ni kwamba fedha ni zao la furaha, na siyo kama wengi wanavyofikiri kwamba furaha ni zao la fedha.

Hivyo basi, usiahirishe furaha yako sasa kwa sababu unatafuta kwanza fedha na unafikiri ukishakuwa nayo basi utapata furaha. Badala yake ishi maisha yako kamili sasa, fanya vile vitu vidogo vidogo vinavyoleta furaha kwenye maisha yako na hivi vitakuwezesha kupata fedha zaidi na kwa kutokutumia nguvu kubwa kama unavyofanya unapokuwa huna furaha.

Usipuuze kitu chochote muhimu kwenye maisha yako kwa sababu unakazana kupata fedha, weka kipaumbele chako kwenye furaha na fedha itakuwa matokeo.

Jipende wewe mwenyewe kwanza, fanya kile unachopenda na zungukwa na wale wanaokupenda, haya yatakuletea furaha na furaha yako itavutia fedha zaidi kwako.

Fuata hili na hutafikia kwenye hali ya wengi ambao wana fedha lakini hawana furaha, wewe tayari unayo kanuni ya kuwa na furaha na kuwa na utajiri kwa wakati mmoja. Ifanyie kazi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; FURAHIA MAGUMU UNAYOPITIA.

“If we didn’t have the struggles that we have had, the challenges, and the pushes, we would never develop our character. Our character is coming from those times when we didn’t believe we could do it, but we did it anyway, and we fought our way through. In that struggle, we developed our character and our strength.” — Brendon Burchard.

Mara nyingi tumekuwa tunakwepa magumu kwenye maisha yetu, tumekuwa tunaomba tusikutane na magumu, kwa sababu tunaona magumu ndiyo kikwazo cha sisi kuwa na maisha tunayoyataka. Lakini hilo siyo sahihi, kama tusingekutana na magumu kabisa kwenye maisha yetu, maisha yangekosa maana na tusingeweza kuwa watu ambao tumekuwa sasa.

Magumu ambayo tumekutana nayo kwenye maisha ndiyo yametufanya tuwe watu ambao tumekuwa sasa. Hivyo badala ya kukataa na kukimbia magumu, tunapaswa kuyakaribisha kwa mikono miwili. Kwa sababu kupitia magumu ndiyo tunakua, na ndiyo tunafikia uwezo mkubwa uliopo ndani yetu.

Kufukuzwa au kukosa kwako kazi huenda kumekufanya ukaweza kuanza biashara yako. Kusumbuliwa kwenye mahusiano yako ya mwanzo na yakavunjika ndiyo kumekupelekea kutengeneza mahusiano mengine bora. Na hata kupata hasara na kufa kwa biashara yako ya mwanzo kumekuwa funzo la wewe kufanikiwa kwenye biashara nyingine.

Tusiogope wala kukimbia magumu, na wala tusiombe kutokukutana na magumu. Badala yake tuombe kuwa imara zaidi ili kuweza kukabiliana na kila gumu tunalokwenda kukutana nalo.

Rafiki yangu mpendwa, hizi ndizo tano za juma hili la nne la mwaka 2018;

 1. Jiulize kwa nini saba ili uweze kujua sababu halisi na ya ndani kwa kila unachofanya.
 2. Jijengee tabia za mafanikio za mamilionea, kwa sababu ni tabia pekee ndiyo zinazowatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa.
 3. Jua vitabu 117 ambavyo vimesomwa na wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA na chagua katika vitabu ambavyo hujasoma na visome mwaka huu 2019.
 4. Fanyia kazi furaha yako na fedha itakuwa zao la furaha hiyo. Usiahirishe furaha mpaka uwe na fedha nyingi, anza kuwa na furaha na fedha zitakuja kwako kwa wingi.
 5. Usiogope wala kukimbia ugumu, ugumu ndiyo unaokufanya wewe kuwa bora zaidi, unaokuwezesha kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako. Utumie ugumu kupiga hatua zaidi.

Ni hayo matano muhimu rafiki kwa juma hili la 4, nikutakie mpangilio bora wa juma la tano na nenda kaliishi kwa mafanikio makubwa sana kwako.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu