Kuweza kupata chochote unachotaka ni kauli kubwa sana ambayo wachache sana wanaweza kuwa na imani nayo. Wengi wanaamini kuna ukomo ambao uko kwao, kwamba kuna vitu hawawezi kuvipata hata iweje.

Lakini ukweli ni kwamba, kwa chochote unachojiambia huwezi kupata au kufikia, kuna mtu alianzia hapo ulipo wewe, na hata wakati mwingine alianzia pabaya zaidi lakini akaweza kufika au kupata anachotaka.

Hivyo anza hapa ukiwa na imani kwamba chochote unachotaka kinawezekana, chochote ambacho unaona mtu mwingine amepata au kufikia basi hata wewe unaweza kupata au kufikia.

Sasa zipo rasilimali nne muhimu ambazo unazo, kama ukizitumia vizuri zitakuwezesha kupiga hatua na kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Rasilimali ya kwanza ni FIKRA ZAKO.

Fikra ndiyo nguzo kuu ya kila unachofanya kwenye maisha, chochote ulichonacho kwenye maisha na popote ulipofika, ni matokeo ya fikra zako. Fikra zetu ndiyo zinavuta chochote ambacho tunacho kwenye maisha yako.

Hivyo tumia fikra zako kukufikisha kule unakotaka kufika, kwa kuwa na taswira ya kule unakotaka kufika na kuifikiria kwa muda mrefu. Muda wote fikiri chanya juu ya kile unachotaka na jione kama tayari umeshakipata.

Usiruhusu fikra hasi juu ya kile unachotaka zikutawale, fikra hizi zinapoingia zing’oe haraka sana kwa kuweka fikra chanya.

Mara zote fikiri kile unachotaka na utaziona fursa zaidi ya kuweza kukifikia.

Rasilimali ya pili ni HISIA ZAKO.

Hisia zetu zina nguvu ya kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu. Ni kupitia hisia zetu ndiyo miili yetu inapata msukumo wa kuchukua hatua fulani. Ukiwa na hisia za mapenzi utasukumwa kufanya kitu cha kukamilisha hisia hizo. Na ukiwa na hisia za chuki mwili wako utatengeneza njia ya kukikwepa na kukikataa kile unachochukia.

Tengeneza hisia kali za mapenzi kwa kile unachotaka, kila unapofikiri kuhusu kile unachotaka, changanya na hisia za kukipenda na kutamani sana kuwa nacho. Kwa kuwa na hisia chanya na kali juu ya kile unachotaka, mwili unapata msukumo zaidi wa kupata unachotaka.

Kinachowafanya baadhi ya watu wawe tayari kufanya kazi zaidi bila ya kuchoka ni miili yao kusukumwa na hisia walizonazo juu ya kupata wanachotaka.

Rasilimali ya tatu ni MANENO.

Maneno unayotumia yana nguvu kubwa sana kwenye maisha yako na hata matokeo unayopata. Ukitumia maneno hasi na ya kukatisha tamaa hutakuwa na hamasa ya kuchukua hatua zaidi. Lakini ukitumia maneno chanya na yenye kutia moyo utapata hamasa ya kuchukua hatua zaidi.

Maneno unayotumia kwako na kwa wengine yana mchango mkubwa sana wa pale mtu anapofika. Hivyo kazana sana kuepuka kujiambia kauli hasi au kusikiliza kauli hasi za wengine. Mara zote tumia maneno chanya na zungukwa na wale wanaotumia maneno chanya.

Rasilimali ya nne ni MATENDO.

Hatua unazochukua ndiyo zinaamua unafika wapi kwenye maisha. Haijalishi una fikra chanya kiasi gani, au hisia zako zinausukuma mwili kiasi gani, na hata kama unatumia maneno chanya mara zote, kama huchukui hatua sahihi za kukufikisha kule unakotaka kwenda, hutaweza kufika huko.

Hivyo lazima uwe mtu wa kuchukua hatua sahihi kulingana na kile unachohitaji kwenye maisha yako. Lazima ujitume kwa kwenda hatua ya ziada. Lazima ukazane kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Na ni muhimu utoe thamani kubwa zaidi kupitia unachofanya. Kwa kuwa na matendo sahihi na yenye kutoa zaidi, utaweza kufika na kupata chochote unachotaka.

Rafiki, hizo ndizo rasilimali nne ambazo zipo ndani yako, ambazo unaweza kuanza kuzitumia leo na zikakuwezesha kupata chochote unachotaka au kufika kokote unakotaka kufika.

Zitumie rasilimali hizi vizuri ili uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha