Kabla hujafanikiwa, watu wengi hawatasumbuka na wewe, unaweza kuishi utakavyo na ukasema chochote utakacho na watu watakupuuza tu. Kwa sababu huna mafanikio makubwa wengi hawakupi uzito, na chochote utakachosema hawatasumbuka nacho. Kwa kifupi kabla hujafanikiwa unakuwa na maisha huru zaidi inapokuja kwenye mahusiano yako na watu wengine.
Lakini unapofanikiwa, mambo yanabadilika, watu wanaanza kukufuatilia zaidi wewe, kila unachosema au kufanya kinachukuliwa kwa uzito. Unaweza kusema kitu kwa utani na watu wakakichukulia kwa uzito mkubwa sana. Unapokuwa na mafanikio makubwa, watu wanakufuatilia zaidi na kila unachofanya kinamulikwa na kutafsiriwa na kila mtu kwa namna wanavyofikiri wao. Kwa kifupi unapofanikiwa unakosa sehemu kubwa ya uhuru wako wa kimaisha, pale inapokuja kwenye mahusiano yako na wengine.
Sasa unapofanikiwa, yapo makundi matatu ya watu yatakayojitokeza kwenye maisha yako. Kama huyajui makundi haya yanaweza kuwa kikwazo kwa mafanikio yako. Lakini kwa kuyajua hayatakusumbua hata kidogo.
Kundi la kwanza ni la watu ambao watatamani sana kuwa na mafanikio uliyonayo. Hawa ni wale wanaotamani kuwa kama wewe, lakini hawapo tayari kuweka kazi ambayo wewe umeweka. Hivyo hawa watakuwa wanatafuta njia za mkato za kufika ulikofika wewe. Na wakati mwingine watataka wewe uwawezeshe kufika pale ulipofika, bila ya wao kuumia kama ulivyoumia wewe. Waelewe hawa na achana nao, usikubali wakusumbue kabisa.
Kundi la pili ni la watu ambao wanapenda kujifunza kutoka kwako, hawa ni watu ambao wapo tayari kuweka juhudi ulizoweka ili nao wapige hatua. Hawa wanajua hakuna njia ya mkato bali kuweka juhudi na wanakuwa tayari kujifunza kwa juhudi ulizoweka. Watu hawa wasaidie kwa kuwashauri vyema na kuwapa moyo ili wachukue hatua na kufanikiwa.
Kundi la tatu ni la watu ambao watakuchukia kwa mafanikio yako, hawa ni wale ambao wanakuonea wivu kwa mafanikio uliyonayo. Hawa wanaamini umefanikiwa kwa bahati tu na hakuna chochote kikubwa ulichofanya. Watu hawa wanaamua kukuchukia bila ya sababu yoyote, ila tu wanakuchukia kwa kuwa umefanikiwa kuliko wao. Watu hawa achana nao kabisa na wasikuumize kwa namna yoyote ile. Jua hayo ni matatizo yao binafsi na yasikusumbue.
Yajue vizuri makundi haya matatu ya watu na kila unayekutana naye kwenye maisha yako jua yupo kundi gani ili ujue hatua sahihi za kuchukua kwake.
Mafanikio ni mazuri na tunayapigania, lakini huwa yanakuja na majukumu yake ambayo ni kama haya ya mahusiano yetu na wengine kubadilika. Usiyachukie mafanikio kwa sababu ya watu kubadilika. Badala yake waelewe na chukua hatua sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,