Yapo mazoezi manne muhimu sana yatakayokuwezesha kujiimarisha kifedha. Kwa kufanya mazoezi haya utaweza kuongeza kipato chako bila ya kujali ni nini unachofanya kwa sasa.
Zoezi la kwanza ni mategemeo chanya. Watu wengi wamekuwa wanafanya kitu au kuomba kitu, lakini ndani yao wanajiambia hawatapata. Wanakuwa na matarajio hasi kwamba hawatapata au hawatakubaliwa. Hivyo inapotokea wanakutana na kikwazo kidogo, wanakubaliana nacho na kutokusukuma zaidi. Inapokuja kwenye swala la fedha, mara zote kuwa na mategemeo chanya, mara zote jiwekee kwamba utapata kile unachotaka, na hivyo ndivyo itakavyokuwa.
Zoezi la pili ni imani hai. Hapa unahitaji kuwa na imani hai na isiyoyumbishwa juu yako binafsi na juu ya kile unachofanya. Amini sana kwenye kazi au biashara unayofanya na amini kile unachotoa kitamsaidia yule anayekilipia. Unapojiamini na kuamini kwenye kile unachofanya, unawafanya wengine nao waamini na kuwa tayari kukulipa kwa kufanya kitu hicho.
Zoezi la tatu ni shukrani isiyo na kikomo. Unapaswa kushukuru kwa kila jambo kwenye maisha yako, na kadiri unavyoshukuru, ndivyo unavyojijengea nafasi ya kupata kilicho bora zaidi. Hata kama unakutana na magumu kiasi gani, angalia upande mzuri wa kila ugumu na shukuru kwa uzuri huo. Utajikuta unakaribisha uzuri zaidi na zaidi.
Zoezi la nne, toa thamani ya juu mara zote. Kwenye kila unachofanya, toa thamani ya juu sana, fanya kwa viwango vya juu mno. Mara zote jikumbushe kwamba kiwango cha fedha ulichonacho sasa ni matokeo ya thamani unayozalisha, hivyo kupata fedha zaidi lazima uzalishe thamani zaidi.
Fanya mazoezi haya manne kila siku na utapiga hatua sana kifedha. Uzuri mazoezi haya hayahitaji cha ziada ili kuanza, unaweza kuanza kuyafanya sasa, kwa hapo hapo ulipo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,