Jambo kubwa na linalosikitisha kwenye maisha ni pale watu ambao wapo kwenye njia sahihi, wanakubali kupotezwa na wale ambao hawapo kwenye njia sahihi.

Hivi ndivyo ambavyo watu wengi wamekuwa wanapotezwa na kuondolewa kwenye njia ya mafanikio makubwa.

Mtu anakuwa na ndoto kubwa, anajiweka malengo na mipango na anaanza kufanyia kazi malengo hayo, na hapo ndipo anapokutana na watu ambao hawana ndoto yoyote kubwa, hawana malengo wala mipango na wanaanza kuwa washauri wazuri kwake.

Watu hao ambao hawajui wapi wanakwenda na maisha yao, wanapata nguvu ya kuwashauri wale wanaojua wanaenda wapi na maisha yao, na bora wangekuwa na ushauri mzuri. Ushauri wanaotoa unakuwa wa kukatisha tamaa na kuwarudisha nyuma.

Mtu ambaye hajawahi kufanya jambo lolote kubwa anakuwa na nguvu ya kumshauri mtu kipi kinawezekana na kipi hakiwezekani. Mtu ambaye hajui wapi anakwenda na maisha yake anathubutu kumshauri mtu anayejua anakokwenda kwamba anakosea kwa kuchagua kwenda huko.

Hapa tunaweza kusema mwenye kosa ni yule asiyejua anakokwenda, lakini makosa makubwa yanakuwa ya yule anayejua anakokwenda lakini bado anamsikiliza yule asiyejua anakwenda wapi.

Rafiki, usikubali kupotezwa na wale waliopotea, kuwa makini sana na chagua nani unayemsikiliza kwenye maisha yako. Hata kama mtu ana ushauri mzuri kiasi gani, kama hajui wapi anaenda na maisha yake, kama hayupo kwenye njia sahihi usimsikilize, ataishia kukurudisha nyuma.

Naomba unielewe sana kwenye hili na uwe mkali sana kwenye kuchagua nani wa kumsikiliza, maana watu wamekuwa wanasikiliza kila mtu wakifikiri watapata mawazo mazuri kutoka kwa wengine. Hakuna wazo zuri unaloweza kupata kwa mtu ambaye hajui anaenda wapi na maisha yake.

Na uelewe sijasema uwasikilize waliofanikiwa tu, bali nasema wasilikize wanaojua wapi wanakwenda na maisha yao. Kitendo tu cha mtu kujua anakwenda wapi na maisha yake na kusimamia hilo, kinamtenganisha na wengi ambao wanapelekwa tu na maisha yanavyokwenda badala ya kuyaishi maisha kwa kwenda wanakotaka wao.

Waliopotea wanapenda kupotea na wengine, kuwa makini sana usikubali kupotezwa na wale waliopotea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha