Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa naweka muda na nguvu kubwa katika kutoa mafunzo ambayo yatatuwezesha kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yetu.
Kwa sababu naamini kwenye kanuni hii muhimu sana; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.
Kama hutaanza na maarifa sahihi, hatua zozote unazochukua zitazidi kukupoteza.
Na kama utakuwa na maarifa sahihi lakini usichukue hatua, hauna tofauti na asiyejua chochote.
Ndiyo maana nimekuwa nasisitiza sana vitu hivyo viwili kwa pamoja kama kweli mtu unataka kupiga hatua kwenye maisha yako.
Lakini nimeona wengi wakiishia njiani kwa sababu mbalimbali.
Wapo ambao wanaanza na hamasa kubwa ya kujifunza na kuchukua hatua, lakini baada ya muda hamasa ile inazima na wanarudi kwenye mazoea yao.
Na hapa ndipo nilipotafakari kwa kina na kugundua tatizo lipo kwenye vitu viwili ambavyo watu wamekuwa hawajitoi ili kuhakikisha maarifa wanayopata yanawasaidia kweli.
Hapa nakwenda kukushirikisha vitu hivyo viwili ambavyo unapaswa kujitoa kupitia vitu hivyo ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kupitia maarifa ninayokushirikisha kila siku.
KITU CHA KWANZA; MUDA.
Lazima ujitoe kwa muda, lazima uweke muda wa kujifunza na lazima uweke muda kwenye kutekeleza yale uliyojifunza.
Zama hizi za kelele watu hawana muda kabisa, hata kusoma makala kama hii watu wengi wanaona ni ndefu na hawana muda. Badala yake watakimbilia kwenye mitandao ya kijamii kuanza kufuatilia maisha ya wengine na huko watapoteza muda mwingi mno.
Rafiki, ni lazima ujitoe kwa muda, lazima utenge muda wa kujifunza kila siku, tena ukiwa na utulivu wa hali ya juu na hata kutafakari baada ya kuwa umejifunza.
Kama huwezi kuwekeza muda wa kujifunza na kuyafanyia kazi yale unayojifunza, hakuna maarifa yanayoweza kukusaidia.
SOMA; Fanya Mambo Haya 19 Pekee Kila Siku Na Mwaka 2019 Utakuwa Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.
KITU CHA PILI; FEDHA.
Fedha ni kitu kingine muhimu unachopaswa kujitoa nacho ili uweze kunufaika na maarifa mbalimbali ninayokushirikisha.
Mara nyingi sisi binadamu tumekuwa hatuthamini vitu tunavyopata bure, hata kama vina thamani kubwa. Ila tunapowekeza fedha zetu kwenye kitu, fedha ambazo tumezipata kwa uchungu, tunathamini zaidi vitu hivyo.
Hivyo kama unataka mafunzo haya yawe na manufaa kwako, kama unataka kujisukuma kufanyia kazi kila unachojifunza basi wekeza fedha. Jitoe kifedha kuhakikisha unapata msukumo wa kutumia kila unachojifunza ili kupiga hatua zaidi.
Unapojitoa kifedha unakuwa na pengo la kuziba na utakazana kutumia mafunzo haya kuziba pengo hilo. Pia unapowekeza fedha, utakazana kutenga muda wa kufanyia kazi pia.
Rafiki, nimekushirikisha vitu hivi viwili kwa sababu kwa sasa nawaepuka sana watu ambao hawawezi kuwekeza vitu hivyo viwili kwenye mafunzo ninayotoa. Kwa zaidi ya miaka mitano ambayo nimekuwa natoa mafunzo haya, nimejifunza kwa mtu ambaye hayupo tayari kuwekeza muda na fedha ili kupata mafunzo yatakayomwezesha kupiga hatua basi hakuna kikubwa kinaweza kutokea kwenye maisha yake.
Natoa muda wangu na nguvu zangu kwa wale ambao wapo tayari kupiga hatua, wale ambao wapo tayari kuwekeza vitu hivyo viwili, muda na fedha. Na kama wewe ni mmoja wa watu hao karibu sana tuendelee kuwa pamoja.
Lakini kama huna dakika 10 mpaka 30 za kutenga kila siku kwa ajili ya kujifunza, kama huwezi kununua kitabu hata cha shilingi elfu 5 na ukajisomea, wewe hatuwezi kwenda pamoja na sina njia nyingine zaidi ya kukusaidia.
Kushindwa kutenga muda na fedha kwa ajili ya ukuaji wako binafsi ni kuchagua kuwa na maisha magumu kwenye zama hizi ambazo fursa ni nyingi na kila mtu anaweza kufanya kila kitu.
Kwa wale wenye muda na kuwa tayari kuwekeza fedha ili kupata mafunzo ninayotoa hakikisha unajiunga na KISIMA CHA MAARIFA kama bado hujafanya hivyo, kwenye KISIMA naweka nguvu kubwa ya kushirikisha maarifa bora kabisa ya kupiga hatua, usipitwe na haya mazuri.
Karibu sana rafiki tuendelee kuwa pamoja, kama una muda na fedha za kuwekeza kwenye ukuaji wako binafsi.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu