“Don’t be bounced around, but submit every impulse to the claims of justice, and protect your clear conviction in every appearance.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.22
Tumeiona siku nyingine nzuri sana leo mwanamafanikio.
Ni jambo la kushukuru sana kuiona siku hii mpya na ya kipekee.
Na shukrani iliyo bora ni kuiishi siku hii kwa ubora wa hali ya juu, kufanya kile kilicho sahihi na kukifanya kwa ubora wa hali ya juu, kwenda hatua ya ziada kila wakati.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; DHIBITI MIHEMKO YAKO….
Kwa walio wengi, maisha ni kama bembea, dakika moja wako juu, dakika nyingine wako chini kabisa.
Kinachokwenda juu na chini kwa mbadiliko huu ni hisia ambazo watu hao wanakuwa nazo, mihemko ambayo wanashindwa kuidhibiti.
Kitendo cha kuwa juu na chini kila wakati kinachosha sana, kinamfanya mtu asitabirike na pia ashindwe kufanya maamuzi yenye msimamo.
Kwani jambo linaweza kutokea akiwa na hisia za juu akaamua hivi, jambo hilo hilo likatokea akiwa na hisia za chini na akaamua vingine.
Sasa hayo siyo maisha yenye utulivu, kama huwezi kudhibiti mihemko yako, hata watu watakuwa wanakitega, wanachochea hisia kwako ili ufanye maamuzi ambayo yatawanufaisha wao.
Unahitaji kushika hatamu ya maisha yako, kudhibiti kila aina ya mhemko, kuwa na chujio la kila hisia unazokuwa nazo. Na mara zote kufanya maamuzi ukiwa na utulivu wa hisia.
Unapojikuta kuna kitu iimetokea na kimechochea sana hisia zako, jiulize je kitu hicho ni muhimu sana? Je hatua ipi sahihi ya kuchukua.
Na muhimu zaidi, usikimbilie kufanya maamuzi yoyote, tulia kwanza. Kwa kutulia kwako hisia zitashuka na utaona jambo hilo kwa upande mwingine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kudhibiti hisia na mihemko yako ili uweze kufanya maamuzi bora kabisa.
#DhibitiHisiaZako #FikiriKablaYaKuamua, #TunzaNguvuZakoKwaYaliyoMuhimu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha