Kwenye dunia ya sasa, karibu kila mtu anasubiri kuambiwa nini cha kufanya, jinsi gani ya kufikiri na kufanya,  na hata jinsi gani ya kujisikia kwenye siku zao na hata kile ambacho wanafanya.

Ni kama dunia nzima inaendeshwa na mfumo mmoja ambao inabidi kila mtu ajihusishe nao ndiyo ajione wa kawaida, ajione amekamilika, kwa sababu anafanya kile ambacho kila mtu anafanya.

Mtandao wa intaneti umefanya watu kuwa tegemezi kwa wengine kwa namna ya kuendesha maisha yao.

Watu wengi kwa sasa hawawezi kufanya maamuzi ya kufanya kitu kama hakuna wengine wanaozungumzia kitu hicho mtandaoni. Watu wanataka mpaka wasome kwa wengine wanaofanya au waone wengine ambao wameweka kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanafanya.

Lakini hivi sivyo ukuu unakuja, hivi sivyo unavyoweza kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Hutapata mafanikio makubwa kwa kusubiri uambiwe nini cha kufanya, kwa kusubiri wengine wafanye na wewe ndiyo uige.

Ukuu unakuja kwa kuchukua hatua, kwa kujua kipi unataka kufanya na kukifanya, hata kama hakuna anayefanya au kuzungumzia. Na hata kama utakosea kwenye kuchukua hatua hizo, utajifunza na kuwa bora zaidi.

Usiogope kuonekana wa tofauti na wala usiogope kukosea, jua kile unachotaka na hatua za kuchukua ili kukipata, na hata kama hakuna mwingine anayefanya au anayewaambia watu wafanye, wewe fanya. Kusubiri mpaka uambiwe nini cha kufanya, au kusubiri mpaka uone wengine wanafanya ndivyo ufanye ni kujichelewesha na kujirudisha nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha