Mafanikio ni sawa na kupanda ngazi, na kila ngazi unayopanda unajisogeza karibu zaidi na mafanikio yako. Hivyo ili kufika kwenye kilele cha mafanikio, lazima uwe tayari kupanda ngazi zote. Kwa sababu kila unapopanda ngazi moja, nyingine inajitokeza mbele yako. Na habari mbaya ni kwamba hakuna lifti, ni lazima uzipande ngazi.

Ngazi za kuelekea kwenye mafanikio makubwa ni kushindwa, kila unaposhindwa unakuwa umekutana na ngazi ambayo itakufikisha kwenye mafanikio ya juu zaidi ya ulipo sasa. Kama utavuka kushindwa huko na kuendelea mbele, basi unakuwa umeipanda ngazi. Lakini kama utakubali kushindwa huko kuwe sababu ya wewe kutokuendelea zaidi utakua umeshindwa kupanda ngazi na utabaki pale ulipo sasa.

Kila unaposhindwa unakuwa umekutana na ngazi ya kukufikisha juu zaidi. Na siyo kwamba ukipanda ngazi hiyo umemaliza, kwamba hutakutana na kushindwa tena. Badala yake unakuwa umejiandaa tu kukutana na kushindwa kwingine zaidi, ambapo ni ngazi ya kwenda juu zaidi.

Ili uweze kuzipanda ngazi hizi za mafanikio mpaka kufika kileleni unahitaji kuwa na sifa kuu mbili;

Moja unapaswa kuwa na subira, kwa sababu chochote unachotaka kinahitaji muda, kama una haraka hutaweza kupanda kila ngazi mpaka kufikia mafanikio makubwa. Kama nilivyokuambia, hakuna lifti, ni kupanda ngazi moja baada ya nyingine.

Mbili unapaswa kuwa na unyenyekevu, kwa sababu lazima ukubali kupokea hali ya kushindwa na kuifanyia kazi ili kuivuka. Kama utakimbia kushindwa, kama utaona hustahili kushindwa, hutaweza kuvuka kushindwa unakokutana nako na hilo litakuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio ya juu.

Kupokea kushindwa na kuwa na subira katika kufikia mafanikio makubwa ni silaha mbili ambazo zitakuwezesha kuzipanda ngazi za mafanikio mpaka kufika kileleni.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha