Zipo sababu nyingi sana za wewe kufanya mambo sahihi, kuwa mwema kwa wengine na kufanya kila ambacho umepanga kufanya.

Lakini moja ya sababu kubwa, na ambayo inaweza kukusukuma zaidi ni kufikiria huenda nafasi uliyonayo sasa ndiyo ya mwisho kwako.

Kwa kujua kwamba hutapata nafasi nyingine ya kufanya kazi au biashara yako, je utaifanyaje saa? Kwa kujua ya kwamba hutakutana tena na mtu kwenye maisha yako yote, je utachukuliaje wakati ulionao sasa?

Je utaahirisha kazi yako na kujiambia utafanya kesho wakati unajua leo ndiyo nafasi ya mwisho kwako?

Na je utamkasirikia mtu na kujiambia hutaweza kumsamehe kama unajua ukiachana naye tu hapo hapo anafariki, au wewe unafariki?

Huwa tunatengeneza matatizo kwa kufikiri tuna muda wa kutosha wa kuyatatua, lakini pale inapotokea kwamba hatuna muda, tunalazimika kufanya kila kitu kwa wakati tulionao.

Sasa wote tunajua kuna wakati utakuwa wa mwisho kwetu, huenda ni leo, huenda ni siku zijazo, hakuna ajuaye lini, lakini tuna uhakika wakati huo wa kufanya kitu kwa mara ya mwisho unakuja.

Sasa huoni kama maisha yako yatakuwa bora sana kama utachukulia kila unachofanya kama wakati wa mwisho kwako kukifanya, na hapo ukifanye kwa ubora wa hali ya juu sana.

Kwa kuiendea siku yako kama ya mwisho, utakamilisha yale muhimu zaidi kwako, utaondokana na kila aina ya kelele na mahusiano yako na wengine yatakuwa bora sana.

Hili ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako, anza kuliishi leo ili kuboresha maisha yako.

Fanya kila fikra zako kuwa fikra za mtu ambaye hana tena muda mwingine wa kufanya kile anachofanya, na hivyo inabidi akifanye kwa ubora sana, maana hatapata tena nafasi hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha