Ni kujilinganisha na watu wengine.

Unapojilinganisha na watu wengine, unajishusha chini au kujipandisha juu kwa namna ambayo siyo sahihi kwako.

Ukijilinganisha na walio juu yako utajiona wewe hujafanya chochote na hivyo kujiikia vibaya sana.

Ukijilinganisha na walio chini yako utajiona umefanya makubwa sana na kuridhika na kuanza kupumzika.

Kujilinganisha ni njia rahisi kwako kujiangusha na kujikatisha tamaa mwenyewe, kwa sababu hakuna yeyote anayefanana na wewe kwa kila kitu. Ni sawa na kulinganisha embe na chunga, yote ni matunda, lakini yanatofautiana sana.

Na kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, wengi wanakuza maisha yao kuliko uhalisia, hivyo kama unatumia mitandao kuona wengine wamepiga hatua zaidi na wanayafurahia maisha yao kuliko wewe, unajidanganya na kujiuliza. Wengi wanaweka sehemu ndogo sana ya maisha yao mtandaoni, sehemu kubwa na ngumu hutaiona.

Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, kwa chochote ambacho unajiona uko vizuri au umefanikiwa sana, kuna wengi ambao wako vizuri zaidi yako na wamefanikiwa sana kuliko wewe.

Hivyo lengo lako siyo kuwashinda wengine wote, lengo lako ni kuwa bora zaidi leo kuliko jana, na ukifanyia lengo hili kazi, na ukaacha wengine wafanye yao, utaweza kupiga hatua sana kwenye maisha yako na kuwa na utulivu mkubwa na kutokukata tamaa.

Jilinganishe wewe na wewe mwenyewe, angalia unaweza kuwaje bora leo kuliko jana na siyo kuwa bora kuliko wengine wote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha