“If someone asks you how to write your name, would you bark out each letter? And if they get angry, would you then return the anger? Wouldn’t you rather gently spell out each letter for them? So then, remember in life that your duties are the sum of individual acts. Pay attention to each of these as you do your duty . . . just methodically complete your task.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.26

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni nafasi nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIFANYE MAMBO KUWA MAGUMU KULIKO YANAVYOPASWA KUWA…
Tunaweza kusema maisha ni rahisi sana kama mtu utachagua kutokuyafanya magumu.
Wewe mwenyewe umekuwa unayachagua kuyafanya maisha yako kuwa magumu pale unapokasirishwa na vitu vidogo vidogo, ambavyo kama ungeviacha vipite ungebaki na amani ya moyo.

Kuna wakati watu wanakufanyia vitu ambavyo vinaweza kukukasirisha sana, na ukaona ni haki yako wewe kukasirika. Lakini kukasirika kwako kunakuumiza wewe zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Jifunze kuacha vitu vidogo vidogo vipite na usiruhusu amani na utulivu wako wa moyo uvurugwe na vitu ambavyo ni vya kupita.
Na kama utafikiri kwa kina, utagundua kila kitu ni cha kupita na hakuna chochote kinachowtahili uzito wa kuvuruga utulivu wako.

Maisha yako ni matokeo ya namna unavyoyachukulia mambo madogo madogo unayofanya na yanayotokea kwenye maisha yako.
Kama unaruhusu kila jambo likuvuruge, utaishia kuwa na maisha ya hovyo sana na yasiyo na utulivu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokuruhusu mambo madogo madogo yavuruge siku yako. Siku ya kulinda amani na utulivu wa akili na nafsi yako.
#UsisumbukeNaMadogo, #LindaUtulivuWaNafsi, #KilaKituKinapita

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha