Kuna mafanikio na mafanikio makubwa.

Pale unapokuwa kwenye asilimia 5 ya juu zaidi ya wengine, hapo umefanikiwa. Lakini unapokuwa kwenye asilimia 1 ya juu ya mafanikio, hapo una mafanikio makubwa na ya viwango vya juu.

Sasa kinachokufikisha kwenye asilimia 5, siyo kitakachokufikisha kwenye asilimia 1 ya mafanikio.

Utafika kwenye asilimia 5 kwa kubadili mtindo wako wa maisha. Kwa mfano kama ukianza kuamka asubuhi na mapema kuliko ulivyozoea, ukaweka juhudi kwenye kazi zako, ukajiwekea akina na kuwekeza, ukatumia vizuri muda wako na kutengeneza mahusiano bora na wengine, utaweza kufika kwenye asilimia 5 ya waliofanikiwa.

Lakini kubadili mtindo wa maisha pekee hakuwezi kukufikisha kwenye asilimia 1, unahitaji mabadiliko mengine makubwa zaidi kufika kwenye asilimia hiyo moja.

Kufika kwenye asilimia moja ya mafanikio makubwa unahitaji kubadilika wewe kama wewe, unahitaji mabadiliko makubwa ya kinafsi, unahitaji kuwa mtu mpya. Kwa kifupi unahitaji kufanya mapinduzi makubwa ndani yako. Unapaswa kubadili kabisa namna unavyofikiri na jinsi unavyochukulia mambo. Unapaswa kujiona wewe na kuona mazingira yanayokuzunguka kwa namna tofauti. Hapa unaacha kufuata sheria za wengine na kutengeneza sheria zako binafsi, unakuja na uvumbuzi wa tofauti kabisa.

Anza na mafanikio, anza kuziishi sheria za wengine ili kupiga hatua na kufika kwenye mafanikio. Na ukishafika kwenye mafanikio, hapo sasa fanya mapinduzi makubwa ndani yako ili uweze kufika kwenye mafanikio makubwa zaidi. Badilika kabisa ili uweze kuipa hii dunia kitu kipya, kitu ambacho hakijawahi kuonekana na hapo ndipo utayafikia mafanikio makubwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha