Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha na kuwa kikwazo kwetu kufikia mafanikio makubwa. Changamoto ni sehemu ya maisha yetu na hazitakuja kukoma, hivyo njia pekee ya kuzikabili ni kuzitatua kabla hazijawa kikwazo kikubwa kwetu.

Leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi mtu unavyoweza kuituliza fedha unayopata ili uweze kupiga hatua kwenye maisha yako.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Na leo wasomaji wenzetu wawili wameomba ushauri unaofanana juu ya hili;

“Nimefanya sana kazi sehemu moja kwa zaidi ya miaka 4 sasa ila kila nikipata fedha haikai nalipwa kiasi cha laki mbili natamani kupiga hatua nifanye nini” – David G. M

“Napata fedha napanga kufanya biashara zinakwisha bila kufanya kitu” – Jovitus J. N.

Kama ambavyo wasomaji wenzetu wameomba ushauri kuhusu eneo la fedha, ni wengi ambao wamekuwa wanakutana na changamoto hii ya fedha kutokukaa. Mtu unafanya kazi sana, unapata fedha lakini yote inaisha na hubaki na chochote. Miaka inaenda na hakuna hatua yoyote ambayo mtu unapiga.

Kabla hatujaingia kwenye hatua za kuchukua ili kutuliza fedha unayoipata, napenda nikupe ukweli halisi kuhusu fedha, ambao unapaswa kuujua kama unataka kupiga hatua kifedha. Kama una kazi inayokuingizia kipato, na hata kama ni kidogo kiasi gani, kama hujaweza kupiga hatua kifedha ni matatizo yako mwenyewe. Tatizo siyo kazi na wala tatizo siyo kipato kuwa kidogo, bali wewe ndiye tatizo. Na ni lazima ulijue tatizo ili uweze kulitatua, kama utakataa wewe siyo tatizo, utaendelea kubaki pale ulipo sasa.

Kama una kipato na hujapiga hatua tatizo ni lako kwa sababu kinachomwezesha mtu kupiga hatua kifedha siyo kipato anachoingiza, bali namna anavyotumia kipato hicho. Na ndiyo maana kunaweza kuwa na watu wawili, ambao wanafanya kazi sana na kipato chao kinalingana, ila mmoja akapiga hatua na mwingine akashindwa. Tofauti inaanzia kwenye namna ambavyo watu wanatumia kipato wanachoingiza, na siyo kipato chenyewe.

Hivyo eneo la kwanza na muhimu kabisa la kuituliza fedha unayoipata ili uweze kupiga hatua ni kubadili namna unavyotumia kila fedha inayopita kwenye mikono yako.

Kwanza kabisa usikubali fedha yote ipite na ubaki bila ya kitu. Anza kwa mingi mkuu wa kuelekea kwenye utajiri ambao ni KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA. Kwa kila fedha unayoipata, kabla hata hujaanza matumizi, ondoa asilimia kumi ya fedha hiyo na iweke pembeni. Hiyo usiitumie hata kama mambo yanakuwa magumu kiasi gani. Tumia ile inayobaki na kama haitatosha basi fanya kazi zaidi kupata fedha zaidi.

Ukishaweka sehemu ya kipato chako pembeni, jitenganishe nacho. Kuna dhana tunaiita KUTENGENEZA GEREZA LA AKIBA YAKO. Fedha huwa haikosi matumizi, ukiwa na fedha karibu lazima tu utaitumia, mambo yatatokea na utajikuta umelazimika kuitumia. Kuondoa hali hiyo hakikisha unajitenga na akiba hiyo, iweke kwenye gereza, sehemu ambayo huwezi kuitoa kabia hata iweje. Ukishaiweka huko unasahau kama ni fedha yako na kuendelea na maisha yako. Kwa njia hii utaweza kukaa na akiba hiyo kwa muda.

Baadhi ya magereza unayoweza kutumia kuweka fedha zako ni kuwa na akaunti maalumu ya benki ambayo unaweza kuweka tu lakini huwezi kutoa kwa muda fulani. Pia kuna aina mbalimbali za uwekezaji kama wa vipande ambapo ni rahisi kuweka fedha ila kuitoa kuna mlolongo mrefu, ambao utakukatisha tamaa.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuituliza Kila Fedha Inayopita Kwenye Mikono Yako Ili Uweze Kujijengea Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Saa ufanye nini?

Kwa wale wote ambao wamekuwa na changamoto ya kushindwa kuituliza fedha wanayoipata, nashauri ufanye hili bila ya kubadili chochote. Yaani fanya kama ninavyoelekeza hapa.

Kokotoa asilimia kumi ya kipato unachoingiza kwa siku, wiki au mwezi, kulingana na unavyolipwa. Kisha fungua akaunti ya benki ambayo unaweza kuweka lakini huwezi kutoa, benki nyingi zina aina hii ya akaunti, nenda kaulize. Kama akaunti ya benki inashindikana, fungua akaunti ya uwekezaji kupitia UTT (www.uttamis.co.tz).

Baada ya kuwa na eneo hilo la kuweka akiba yako, kila unapopokea kipato chako, kabla ya kutumia, chukua asilimia ile kumi na weka kwenye gereza hilo. Ukishaweka huko sahau kabisa na endelea na maisha yako. Fanya hivyo kwa mwaka mmoja bila ya kugusa kabisa akiba hiyo, na utaona jinsi ambavyo utakuwa umepiga hatua kubwa ukilinganisha na sasa.

Na kama kipato chako hakitoshelezi, usiache kuweka akiba, weka na hapo pata msukumo wa kufanya kazi zaidi ili kuongeza kipato chako.

Fanyia kazi hatua hii muhimu niliyokushirikisha hapa na nipe mrejesho baada ya mwaka mmoja.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog