“Remember to conduct yourself in life as if at a banquet. As something being passed around comes to you, reach out your hand and take a moderate helping. Does it pass you by? Don’t stop it. It hasn’t yet come? Don’t burn in desire for it, but wait until it arrives in front of you. Act this way with children, a spouse, toward position, with wealth—one day it will make you worthy of a banquet with the gods.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 15

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KARAMU YA MAISHA…
Yaendeshe maisha yako kama vile upo kwenye karamu.
Kama kuna kitu kinapitishwa, kinapofika kwako, chukua kwa kiasi. Kama kimekupita usikimbilie kukisimamisha. Na kama bado hakijakufikia usisukumwe na tamaa kukifikia, subiri mpaka kitakapokufikia.
Fanya hivi kwa watoto wako, mwenza wako, nafasi yako na hata kwenye mali na utajiri na utakuwa na utulivu mkubwa sana wa maisha yako.

Tumekuwa tunaharibu utulivu wa maisha yetu kwa kuhangaika na vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu, au vitu ambavyo bado havijawa tayari kwa ajili yetu.
Kama upo kwenye sherehe na upo kwenye mstari wa kwenda kupata chakula, unakuwa na subira na utulivu, ukijua zamu yako itafika na wewe utapata chakula. Mwingine kupita na chakula mbele yako haikufanyi uvuruge utaratibu wa kukaa kwenye mstari kwa kuwa unaona utakosa.
Ni ustaarabu mdogo ambao unaziwezesha sherehe kufanyika kwa amani na utulivu, na mwisho wa siku kila mtu kufurahia.

Peleka ustaarabu huo kwenye maisha yako na utaweza kuwa na maisha yenye amani, utulivu na furaha muda wote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na subira na matumaini kwamba mambo bora yanakuja kwako kwa wakati wake.
#SubiraNiMuhimu, #ZamuYakoItafika, #MaishaYaUtulivuNiBora

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha