Ni mazingira, mara zote mazingira yamekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kubadili tabia.
Huwezi kubadili tabia kama bado utabaki kwenye mazingira ambayo yanashawishi tabia unayotaka kuvunja.
Kwa mfano unataka kuacha kunywa pombe, lakini marafiki zako wote ni wanyaji wa pombe, na mnakutaka kwenye eneo la unywaji wa pombe. Huwezi kabisa kuvunja tabia hiyo ya kunywa pombe.
Mwanzoni unaweza kutumia nguvu kujizuia kunywa, ukaishinda ile tamaa. Lakini akili zetu huwa zinachoka haraka, kadiri unavyokwenda nguvu yako ya ushawishi inapungua na unajikuta ukijiambia nikinywa moja siyo mbaya, unapokuja kustuka umeshalewa tena na kurudi kwenye tabia hiyo.
Kitu cha kwanza kwenye kubadili tabia ni kubadili mazingira. Ondoa kabisa kila hali ambayo inachochea kufanya tabia unayotaka kuifanya. Na weka kikwazo kikubwa kwenye kuifanya tabia hiyo.
Mtu mmoja ambaye alikuwa anapata shida kubwa ya kuacha kutafuna vitu vidogo vidogo ambavyo vinapelekea uzito wake kuongezeka, aliamua kuchukua vitafunwa vyote na kuviweka kwenye dari la nyumba yake. Hivyo pale alipojisikia kutafuna kitu, ilimbidi achukue ngazi, apande darini ndiyo achukue kitu cha kutafuna. Kwa kuweka ugumu huu, aliweza kuvunja kabisa tabia ya kutafuna tafuna vitu.
Kadhalika kwako pia, weka ugumu wa wewe kufikia tabia unayotaka kuacha. Kwa mfano kama unataka kuvunja tabia ya kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii, ondoa app zote za mitandao ya kijamii kwenye simu yako. Na kama unataka kuingia basi inabidi utumie kompyuta. Hilo litakuokolea muda sana kwa sababu unapokuwa huna kompyuta hufikirii kabisa kuhusu mitandao hiyo.
Njia nyingine ni kuzima kabisa mtandao wa intaneti kwenye masaa fulani ya siku yako, hapo hata iweje, hutawasha mtandao kwenye simu au kifaa chako. Hapo pia utapunguza kama siyo kuvunja kabisa tabia ya kupoteza muda kwenye mtandao.
Badili mazingira yao, weka ugumu wa wewe kufanya kile ambacho umezoea kufanya, ambacho unataka kukibadili na itakuwa rahisi kwako kuvunja tabia yoyote inayokuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha hapa nimepata tiba
LikeLike
Karibu.
LikeLike