Pamekuwa na juhudi kubwa kwa wengi kujitofautisha na kazi zao, kwamba wao ni wao na kazi zao ni kazi. Mafunzo mengi yamekuwa yanatolewa ya jinsi ya mtu kujitenganisha na kazi yake, ili kupata mlinganyo mzuri wa kazi na maisha.
Katika juhudi hizi za kujitofautisha na kazi, imepelekea wengi kuchukulia kazi zao kama kitu ambacho inabidi wafanye ili maisha yaende. Siyo kitu ambacho wanakuwa wana hamasa ya kufanya. Na ndiyo maana haishangazi kuwakuta watu wakiwa kazini kimwili, lakini kiakili na kiroho wapo kwingine kabia.
Ni kawaida kumkuta mtu kwenye kazi yake, lakini anatafuta kila sababu ya kukwepa majukumu yake. Anapaswa kutekeleza majukumu yake au kuwahudumia wateja, lakini yupo bize na simu yake au anazurura kwenye mitandao ya kijamii.
Haya ndiyo matunda ya kutaka kujitenga na kazi au biashara ambayo mtu unafanya, unapunguza umakini wako na kuona unachofanya ni cha kupita tu, tena kinakuzuia kuishi maisha yako. Na hili limepelekea wengi kutokuridhishwa na kazi zao.
Ipo njia moja ya wewe kuridhishwa na kazi au biashara ambayo unaifanya. Na njia hiyo ni kuifanya kazi au biashara hiyo kuwa wewe. Kuweka utu wako kwenye kila unachofanya, kuleta utofauti na upekee wako kwenye kila unachofanya.
Unapofanya wewe, unafanya kwa utofauti mkubwa ambao hakuna mwingine anaweza kufanya hivyo. Jali sana kile unachofanya, nenda hatua ya ziada katika kufanya ili kuweza kutoa matokeo ya kipekee.
Unapokuwa kwenye kazi au biashara yako, usione kama ni sehemu ya kusukuma muda upite, bali yaone yale ndiyo maisha yako, kile ndiyo unachopaswa kufanya, ulichochagua kufanya na chenye maana kubwa kwako na wale wanaonufaika nacho.
Kwa kubadili tu fikra zako juu ya kile unachofanya, utaweza kupata matokeo makubwa na ya tofauti kabisa kwenye kazi au biashara unayofanya. Usikubali kufanya kazi au biashara kama kitu cha kupita, bali fanya kama ndiyo maisha yako. Kwa sababu ni kweli, kile unachofanya ndiyo maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,