“Of all the things that are, some are good, others bad, and yet others indifferent. The good are virtues and all that share in them; the bad are the vices and all that indulge them; the indifferent lie in between virtue and vice and include wealth, health, life, death, pleasure, and pain.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.19.12b–13

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari VINAVYOWASUMBUA WENGINE, VISIWE NA TOFAUTI KWAKO…
Vitu vyote tunavyofanya, vimegawanyika katika makundi matatu,
Kundi la kwanza ni mambo mema kufanya, haya ni yale mazuri tunayopaswa kuyafanya na kujipima nayo. Wema upo kwenye hekima, ujasiri, kiasi na haki.
Kundi la pili ni mambo ambayo ni maovu, haya ni yale ambayo hatupaswi kuyafanya na kila siku kukazana kuyaepuka. Uovu upo kwenye upumbavu, udhalimu, hofu na kukosa kiasi.
Kundi la tatu ni mambo yasiyo na tofauti, yaani siyo mema na wala siyo maovu. Haya ni mambo ambayo hakuna ubaya kwenye kuyafanya au kwenye kuwa nayo. Yasiyo na tofauti ni kama utajiri, afya, maisha, kifo, raha na maumivu.

Sasa watu wengi wamekuwa watumwa wa yale yasiyo na tofauti, wanakiwa na tamaa kubwa ya kujikusanyia hayo yasiyo na yofauti au kuyakwepa. Wengi wamekuwa watumwa wa kukimbilia raha na kukimbia maumivu.
Lakini kwako wewe, kama unataka maisha yenye utulivu, basi yasiyo na tofauti yasikusumbue kabisa. Usiwe mtumwa wa kukimbiza hayo, badala yake kazana na yale yaliyo mema.

Ukikazana na mema, utajikuta unapata mengi ya yasiyo na tofauti, bila hata ya kusumbuka nayo.
Mfano ukawa na hekima, ujasiri, kiasi na haki, utakuwa na maisha ya utajiri na yenye afya bora, bila hata ya kuhangaika na vitu hivyo.
Usikubali visivyo na tofauti vikusumbue kama vinavyowasumbua wengi.
Shika hatamu ya maisha yako na kazana na yale yaliyo muhimu zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutosumbuka na yasiyo na tofauti, badala yake kuhangaika na yale mema.
#DhibitiHisiaZako #TawalaFikraZako, #HangaikaNaYaliyoMema

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha