Hii ni kauli ambayo nimekuwa naona inatumiwa na watu wengi sana, wengi wanaitumia kama utani na wengine kama sababu.

Lakini siyo wengi wanaoipa kauli hiyo uzito ambao inastahili.

Kama utaipa kauli hiyo uzito unaostahili, itaweza kukusaidia sana kwenye maisha yako.

Kama kweli unakiri mambo ni mengi na muda ni mchache, hapo sasa unalazimika kujiwekea vipaumbele. Kwa sababu hakuna namna unaweza kufanya mambo hayo mengi kwa muda mchache ulionao.

Hivyo unapaswa kupima kila unachotaka kufanya, na kuona je ndiyo kitu muhimu kabisa unachoweza kufanya kwa muda ulionao? Pale unapokuwa na mengi ya kufanya, lakini muda ni mchache, huna anasa ya kupoteza muda wako kwenye kufanya mambo yasiyo na tija kwako.

Watu wengi wanajidanganya kwamba wanaweza kupata muda wa kuweka kwenye kila kinachopita mbele yao, na hivyo kujikuta siku zinapita na hakuna hatua wanapiga licha ya kuchoka kila siku.

Ukweli ni kwamba, ukipoteza nguvu na muda wako kwa kutaka kufanya kila kinachojitokeza, unakosa nguvu na muda wa kufanya yale muhimu zaidi.

Hivyo jikumbushe kauli hii kabla hujaanza kufanya chochote, kwamba una mengi ya kufanya, lakini muda ulionao ni mchache, je hicho unachotaka kufanya ndiyo kilicho muhimu kuliko vitu vingine vyote ambavyo ungeweza kufanya? Kama jibu ni hapana basi acha mara moja na nenda kafanye kile kilicho muhimu.

Ni kweli mambo ni mengi na muda ni mchache, lakini je unaiishi kauli hii kwa uhalisia au unaisema tu. Jipime kila wakati kwa kauli hiyo na utaweza kutumia muda wako vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha