“Whenever someone has done wrong by you, immediately consider what notion of good or evil they had in doing it. For when you see that, you’ll feel compassion, instead of astonishment or rage. For you may yourself have the same notions of good and evil, or similar ones, in which case you’ll make an allowance for what they’ve done. But if you no longer hold the same notions, you’ll be more readily gracious for their error.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.26
Tumeiona siku nyingine mpya, nzuri na ya kipekee sana kwetu,
Siku ambayo tuna uhuru wa kutumia muda wetu kufanya yale muhimu au kuchagua kuupoteza kwa yasiyo muhimu.
Tunachokwenda kufanya leo, kina maamuzi makubwa sana kwenye maisha yetu ya kesho.
Hivyp itakuwa vyema sana kwako kama utaiishi siku ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA huku ukienda kwa mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA ambavyo vitakuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JIWEKE KWENYE MTAZAMO WA MKOSAJI…
Kuna watu wachache sana ambao wanafanya makosa kwa kukusudia kweli kufanya makosa. Na hawa ni wale ambao iko wazi kwamba wana tatizo fulani kwenye afya yao ya akili.
Lakini kwa walio wengi, tunaweza kusema karibu kila mtu mwenye akili timamu, hakuna anayefanya makosa kwa kukusudia kufanya makosa hayo.
Wengi wanafanya makosa wakiwa na nia njema ya kufanya mambo mazuri.
Kinachofanya wawe wakosaji ni kile wanachofikiri, mtazamo walio nao.
Kwa uelewa na ufahamu wao, wanafikiri wanachofanya ni sahihi, lakini kumbe siyo.
Hivyo kabla hujapatwa hasira na kuwahukumu wale wanaokukosea, hebu kwanza jiweke kwenye mtazamo wao. Jiulize ni kwa namna gani kile ambacho mtu amefanya, ambacho amekukosea, kinaweza kuwa sahihi kwa upande wake, kwa fikra na hisia anazoweza kuwa nazo.
Ukichukua muda kufikiria hili na kujiweka kwenye mtazamo na hisia za anayekukosea, utaishia kuwaonea huruma wale wanaokukosea na hutakuwa na hasira wala vinyongo ambavyo havina maana.
Huwa ni rahisi kwetu kuwasamehe na kuwaelewa watoto pale wanapokosea, na tunajiambia ni utoto unawasumbua. Lakini watu wazima wanapotukosea tunafikiria wamedhamiria, wamefanya kwa makusudi, kitu ambacho siyo kweli wala siyo sahihi.
Angalia kwa kina kila anayekukosea au kufanya ambacho hukutegemea, angalia msukumo wa yeye kufanya na utagundua kwamba hawakufanya kwa kudhamiria, na wakati mwingine, walikuwa na nia njema kabisa.
Kama ukiwapa wengine nafasi unayowapa watoto, nafasi ya kukosea kwa sababu hawajui, hutasumbuliwa na mambo madogo madogo yanayowasumbua wengi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kumchukulia kila anayekukosea kama mtoto ambaye hajui afanyalo, kujitahidi kuelewa msukumo wa yeye kufanya hivyo na kisha kumwelewesha kipi sahihi cha kufanya.
#KukoseaNiUbinadamu, #HakunaAnayekufanyiaMakusudi, #ElewaMtazamoNaHisiaZaWengine
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha