Rafiki, ipo kauli maarufu kwamba hakuna kitu cha bure, kwamba unapoambiwa unapata kitu bure, kuna namna unagharamia kile unachopata bure. Inaweza kuwa kwenye ubora, kwamba unapata kitu bure, lakini hakitakuwa bora kama unavyotaka na huwezi kuhoji kwa sababu umepata bure. Au unaweza kulipa gharama kwenye utu wako, pale unapopata kitu bure, unajiona usiyeweza na unayepaswa kusaidiwa na wengine. Ndiyo maana kama unataka uhuru kwenye maisha, basi epuka sana vitu vya bure na kuwa tayari kulipa gharama.

Kutoka kwenye msingi huo wa hakuna kitu cha bure, mikopo pia inaingia hapo, unapokopa kitu, kuna riba ambayo utalipa. Hata kama unaambiwa mkopo huu hauna riba, au unapewa utumie kwa muda kisha urejeshe, hutakuwa huru kutumia kitu ambacho siyo chako. Huenda ndani yako utajiona wa chini au huenda wale waliokupa kitu wakataka kukupangia namna unavyopaswa kukitumia. Hivyo unapotumia kitu cha mwingine, jua unapoteza uhuru wako.

Sasa riba kubwa sana ipo kwenye mkopo wa muda, na huu unapaswa kuwa nao makini sana. Watu wengi wamekuwa hawajui kama wana mkopo wa muda, achilia mbali kujua kama wanalipa riba kubwa kwa mkopo huo.

Pale unapopanga kufanya kitu leo, lakini ukaahirisha na kusema utafanya kesho, umekopa muda. Sasa riba kubwa ya mkopo huu itakuwa hapo kesho, ambapo badala ya kufanya kitu cha siku mpya unayoanza, inabidi ufanye kitu cha siku ya nyuma, na hivyo muda unapotea huku ukiwa hujapiga hatua yoyote. Hapa unakuwa umepoteza vitu viwili kwa wakati mmoja, muda na nguvu pia.

Epuka sana kuchukua mkopo wa muda, kwa kuwa huu una riba kubwa na itakayokuumiza sana. Kama unapanga kitu kifanye, usikubali kabisa kujiambia utafanya kesho, kitu ambacho unaweza kukifanya leo. Ishi kila siku yako kwa ukamilifu, kwa kutumia kila dakika ya siku hiyo kwa yale ambayo ni muhimu. Usipoteze muda wako wala wa wengine kwa yale yasiyo muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha