Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio yanahitaji timu ya watu, kufikiri kwamba utaweza kufanikiwa wewe mwenyewe, kwa juhudi zako mwenyewe ni kujidanganya. Unahitaji msaada na ushirikiano wa wengine ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Na ukiyaangalia maisha ya wengi waliofanikiwa, wana mtandao muhimu wa watu ambao wamewawezesha kufika pale walipofika. Bila ya mtandao huo, huenda wasingefika pale walipofika sasa.

Nimekuwa nakushirikisha kauli moja muhimu sana kuhusu madhara ya wale wanaokuzunguka kwenye mafanikio yako. Jim Rhon alituambia ya kwamba maisha yako ni wastani wa watu watano unaokuwa nao kwa muda mwingi. Hii inazidi kuonesha umuhimu wa watu kwenye mafanikio yetu. Kama tutazungukwa na watu waliofanikiwa, na sisi pia tutafanikiwa. Tukizungukwa na watu walioshindwa, na sisi pia tutashindwa. Na wala huhitaji kujaribu hili ili kudhibitisha, wewe angalia tu kwenye maisha ya wengine.

network networth

Leo tunakwenda kujifunza watu watatu muhimu sana unaohitaji kuwa nao kwenye maisha yako ili kufikia mafanikio makubwa. Hawa ni watu ambao utaambatana nao kwenye safari ya mafanikio, ambao uwepo wao kwenye maisha yako utakuwa na mchango mkubwa kwako kupiga hatua.

Mtu wa kwanza ni aliyepiga hatua kuliko wewe.

Mtu wa kwanza unayepaswa kuwa naye kwenye maisha yako ni yule ambaye ameshapiga hatua kuliko wewe. Mtu huyu anakuwa amefanikiwa zaidi kuliko wewe, anakuwa ameshafika kule ambapo wewe unatamani kufika.

Mtu huyu atakuwa mwalimu, mshauri, kocha na hata menta kwako kukuwezesha kupiga hatua pia.

Mtu huyu pia atakuwa hamasa kwako kuweza kufanikiwa zaidi, kwa kuona yeye amefanikiwa na kujua namna alivyofanikiwa, utaona kumbe inawezekana na wewe kufanikiwa pia.

Ukishakuwa na mtu aliyepiga hatua kuliko wewe, unapaswa kumwamini na kuwa tayari kujifunza kwake, unapaswa kumtumia kama kipimo cha hatua unazopiga.

Kama bado hujawa na mtu wa aina hii kwenye maisha yako anza kutafuta sasa, angalia kwenye lile eneo ambalo unataka kufanikiwa au kubobea, kisha ona ni watu gani waliopiga hatua zaidi na tafuta ambaye utaambatana naye.

Kwa kuwa watu waliofanikiwa kuliko wewe wana mambo mengi na muda wao ni mchache, unapaswa kutengeneza mazingira ya kila mmoja kunufaika. Isiwe kukutana na mtu huyo ni wewe tu unanufaika kwa kupata ushauri na mwongozo sahihi, bali pia wewe uwe na kitu cha kumsaidia katika mambo anayofanyia kazi. Ukiwa na kitu cha kutoa kwao, mahusiano yenu yanakuwa bora zaidi.

SOMA; Hii Hapa Ni Fursa Kubwa Ya Wewe Na Wengine Kupata Mafunzo Zaidi Kutoka Kwa Kocha Dr Makirita Amani.

Mtu wa pili ni ambaye mpo ngazi moja ya mafanikio.

Mtu wa pili unayepaswa kuwa naye kwenye maisha yako ni yule ambaye mpo ngazi moja ya mafanikio. Mtu huyu mnakuwa mpo kwenye hatua moja ya mafanikio, na hivyo anakuwa kama mshirika wako wa karibu katika safari ya mafanikio. Huyu ndiye mtakayepambana pamoja, ambaye mtakuwa mnapeana hamasa kwa hatua ambazo kila mmoja wenu anapiga.

Kuwa na yule ambaye mpo ngazi moja ya mafanikio ni muhimu, kwa sababu huyu ndiye utakayetumia muda mwingi kuwa naye huku mkibadilishana uzoefu na kushirikishana hatua mnazopiga na changamoto mnazopitia.

Mpaka sasa unapaswa kuwa na watu ambao mpo safari moja ya mafanikio, kama bado basi anza kutengeneza watu hawa. Angalia watu ambao wana kiu ya kupiga hatua kuliko pale ambapo wamefika sasa, kisha tengeneza nao mahusiano ambayo yatawanufaisha wote kwenye safari hiyo ya mafanikio.

Hapa ndipo nguvu ya watu watano wanaokuzunguka inapokuja kwenye maisha yako. Kama utatumia muda wako mwingi na wale ambao wanakazana kufanikiwa, utafanikiwa pia. Lakini kama utatumia muda wako mwingi na walikata tamaa ya mafanikio, hamasa yoyote ya mafanikio iliyopo ndani yako itapotea kabisa.

Mtu wa tatu ni ambaye umemzidi.

Mtu wa tatu unayepaswa kuwa naye kwenye safari yako ya mafanikio ni yule ambaye umemzidi kimafanikio, yule ambaye umefanikiwa kuliko yeye. Mtu huyu atakuwa mwanafunzi kwako, ambaye utakuwa unamfundisha na kumshauri njia sahihi kwake kupita ili afanikiwe. Huyu ni mtu ambaye anatamani kufika pale ambapo wewe umeshafika kwa sasa, lakini bado yupo juu.

Mtu huyu wa tatu ni muhimu sana kwa sababu ipo kauli inayosema hujaelewa kitu mpaka unapoweza kumfundisha mtu mwingine kitu hicho. Hivyo kuwa na mtu ambaye umemzidi, ambaye unamfundisha na kumshauri, itakuwa sehemu nzuri ya kujipima kama kweli unaelewa yale uliyojifunza.

Kadiri unavyoweza kufundisha na kumshauri vizuri yule ambaye yupo chini yako na akaweza kupiga hatua, wewe pia utaweza kupiga hatua zaidi. Usione kama kuwa na mtu unayemfundisha ni mzigo, na wala usisubiri mpaka ufanikiwe sana ndiyo uweze kufundisha wengine. Ukipata mtu mwenye moyo wa kujifunza na kujituma, ambaye kuna hatua umepiga kuliko yeye, mfanye kuwa mwanafunzi wako. Kwa sababu yapo mengine mengi ambayo utajifunza kwake pia.

Rafiki, hao ndiyo watu watatu muhimu sana unaopaswa kuwa nao kwenye safari yako ya mafanikio ili uweze kufanikiwa zaidi. Watu hawa wanaweza kuwa wanabadilika kadiri unavyokwenda, hivyo mara zote angalia fursa za kupata aina hizi za watu ili uweze kuambatana nao na kurahisisha safari yako ya mafanikio.

Kumbuka kila mtu unayempa nafasi kwenye maisha yako, kuna madhara ambayo anayaacha kwenye maisha yako. Hivyo chukulia kwa uzito sana ni watu gani unawaruhusu kwenye maisha yako, na vigezo umeshajifunza hapa, awe ni mtu ambaye ameshafanikiwa kuliko wewe na yupo tayari kukufundisha, au awe ni mtu ambaye yupo ngazi ya mafanikio uliyopo wewe na yupo tayari kushirikiana na wewe, au ni mtu ambaye yupo ngazi ya chini ya mafanikio kuliko wewe na yupo tayari kujifunza kutoka kwako.

Tengeneza timu imara kwa mafanikio yako na utaweza kufanikiwa sana.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO