Unapokuwa ndani ya kundi hupati tena nafasi ya kufikiri, badala yake unachukua fikra za kundi, unafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Hivyo huna haja ya kujiumiza kufanya maamuzi magumu.

Wengi hukimbilia urahisi huu, badala ya kufanya maamuzi magumu wao wenyewe, wanaingia ndani ya kundi na hivyo kufanya kile ambacho kila mtu anafanya.

Lakini hili linakuja na gharama kubwa sana, ambayo ni kukosa uhuru. Unapokuwa ndani ya kundi, na kubeba fikra za kundi kama ndiyo sahihi, unakosa uhuru wa kufikiri mwenyewe na kuhoji vitu.

Mambo mengi yanayofanywa na kundi huwa siyo sahihi au hayana umuhimu, lakini huwezi kuyahoji ukiwa ndani ya kundi. Maana ukihoji ukiwa ndani ya kundi wengine wataanza kukushuku, na kuona huna imani na kundi, wengine watakuita msaliti.

Kuna makundi mengi sana ya kijamii ambayo tunajikuta tupo ndani yake, kuanzia eneo tunaloishi, kabila lako, chama cha siasa, timu unayoshabikia, dini yako, eneo la kazi na jumuia nyingine ndogo ndogo.

Suluhisho la hali hii siyo kujiondoa kwenye kila kundi, kuna manufaa mengi unayapata kwa kuwa kwenye makundi mbalimbali. Suluhisho ni kutokukubali kubeba fikra za kundi kama ndiyo fikra sahihi. Badala yake fikiri kwa akili yako na hoji kila kinachofanywa au kukubaliwa na kundi. Chambua kabisa na ujue kipi sahihi na kipi siyo sahihi. Na huna haja ya kuwaeleza wengine hili, lakini wewe jua kabisa kipi sahihi na kipi siyo sahihi.

Kwa kufikiri mwenyewe na kuhoji kila kinachofanyika au kukubalika na kundi, utakuwa huru, hata kama utafanya kitu, utajua kwa nini unakifanya na utakuwa wazi kama ni kitu sahihi au siyo kitu sahihi.

Usitumie kundi kama sehemu ya kuficha uvivu wako wa kufikiri na kufanya maamuzi magumu. Badala yake tumia kundi kama sehemu ya kujenga uhuru wako, kwa kufikiri na kuhoji kila kinachofanyika na kukubalika, ili uwe na uelewa wa kila unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha