“Today I escaped from the crush of circumstances, or better put, I threw them out, for the crush wasn’t from outside me but in my own assumptions.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 9.13
Siku mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NI MPAKA WEWE UTOE RUHUSA…
Hakuna kitu chochote kinachotokea nje yako ambacho kina nguvu ya kukuvuruga wewe, mpaka pale wewe mwenyewe utakapotoa ruhusa ya kuvurugwa na kitu hicho.
Hata kama yanayotokea ni mabaya na magumu kiasi gani,
Hata kama kila unachogusa kinashindikana,
Hata kama unaowategemea wanakuangusha,
Hata kama kuna watu wanafanya hila ya kukuangusha au kukurudisha nyuma,
Yote haya hayana nguvu ya kukuvuruga wewe kama hutatoa ruhusa.
Wewe ndiye mwamuzi mkuu wa kitu gani kikuvuruge na hivyo pia una nguvu ya kuzuia chochote kile kisikuvuruge.
Chochote kinachokuvuruga na kukusumbua sasa, jua ni wewe umekipa ruhusa, na hivyo unaweza kukinyima ruhusa na maisha yako yakawa bora, licha ya changamoto unazopitia.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutoruhusu chochote kinachotokea kikuvuruge, siku ya kuwa na utulivu mkubwa ndani yako bila ya kujali nini kinaendelea nje.
#MaishaNiKuchagua #DhibitiFikraZako, #FikiriChanya
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha