Moja ya uwekezaji bora kabisa unaoweza kufanya kwenye maisha yako ni kwenye maendeleo yako binafsi.
Kujifunza vizuri vipya ili kuwa bora zaidi kutakuwezesha kupiga hatua sana kwenye maisha yako.
Lakini jua siyo kwamba hili litakusaidia wewe pekee, bali litawasaidia wengine wengi na hata dunia kwa ujumla.
Kama umeajiriwa na ukawekeza kwenye kujiendeleza binafsi, ukatoa huduma bora sana, siyo tu kipato chako kitaongezeka, lakini pia wale wanaopata huduma unazotoa watakuwa na maisha bora kuliko awali.
Kama unafanya biashara na ukawekeza kwenye maendeleo yako binafsi, siyo tu utapata faida kubwa, bali wateja wako watakuwa na maisha bora kupitia kile unachowauzia.
Kwa kitendo cha kuchagua kuwekeza ndani yako, siyo tu unanufaika wewe, bali kila anayekutana na wewe ananufaika na yeye pia anaenda kuwanufaisha wengine. Hata kitendo cha wengine kuona wewe umepiga hatua na wakapata hamasa ya kupiga hatua pia, unakuwa umechangia kwa wao kupiga hatua.
Hivyo unapofanya uwekezaji huu wa kuwa bora zaidi, unapokazana kujifunza zaidi ili kupiga hatua zaidi, jua siyo wewe pekee utakayenufaika na hilo, bali wengi wanaohusika na wewe watanufaika pia.
Kwa maana hii, kujiendeleza binafsi na kuwa bora zaidi kunakuwa wajibu wako mkubwa kwenye maisha na siyo kitu cha kujisikia kufanya. Kwa sababu usipofanya hivyo, siyo tu unajikwamisha wewe mwenyewe, bali unawakwamisha na wengine pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,