Rafiki,
Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa tunafanya kila juhudi kuukimbia ukweli. Kwa sababu ukweli unaumiza na haubembelezi, basi wanadamu tumekuwa hatuupendi. Hivyo tumekuwa tunatafuta kila namna ya kuukwepa au kuuficha ukweli.
Na ukiangalia jinsi dunia inavyokwenda, taasisi nyingi ambazo zina wafuasi wengi, hazijajengwa kwenye misingi ya ukweli. Ukianzia kwenye taasisi kama nchi, mashirika makubwa, dini na hata jamii ndogo ndogo, ukitaka kuchimba ule ukweli wa ndani utagundua kinachowezesha taasisi hizo kuwa na watu wengi wanaozifuata au kuzikubali siyo ukweli, bali jinsi zinavyoweza kuuficha au kuupuuza ukweli.
Lakini ukweli huwa haushindani, badala yake unabaki kuwa ukweli, na baada ya yote, ukweli hushinda mwishoni. Kuukwepa ukweli na hata kuupuuza hakuubadili na ukawa uongo, badala yake ni kujiandaa kwa maumivu ya baadaye.
Hakuna aliyeukimbia, kuuficha au kuupuuza ukweli akabaki salama. Tunaweza kusema mateso mengi ambayo wanadamu tunayapitia chanzo chake kikuu ni kuukimbia ukweli.
Katika makala hii tunakwenda kujifunza kweli tatu chungu ambazo kila mtu anapaswa kuzijua ili awe na maisha yenye utulivu na mafanikio makubwa. Watu na taasisi mbalimbali zinaweza kukuambia kinyume na kweli hizi, lakini shika akili yako na simama kwenye ukweli, kama hutaki kujiumiza baadaye.
UKWELI WA KWANZA; KILA KITU KINABADILIKA.
Kitu pekee ambacho hakibadiliki kwenye haya maisha ni mabadiliko. Kila kitu kinabadilika, hata kama ni taratibu kiasi gani, hakuna kitakachobaki kama kilivyo sasa. Kwa kuanza na mwili wako mwenyewe, unabadilika, ulivyokuwa jana sivyo ulivyo leo na kesho utakuwa tofauti kabisa. Kazi unayofanya inabadilika, biashara unayofanya inabadilika, mahusiano uliyonayo yanabadilika.
Kwa kujua ukweli huu unapaswa kubadilika kila wakati, hupaswi kuzoea na kuridhika na chochote na kuona hapo ndiyo umefika mwisho. Jua mabadiliko yanakuja, hivyo kuwa mbele ya mabadiliko. Anza kubadilika wewe mwenyewe kabla mabadiliko hayajakulazimisha ubadilike.
Kwenye maisha wale wanaobadilika kabla ya ambadiliko wananufaika sana, lakini wale wanaolazimishwa kubadilika na mabadiliko wanapoteza.
Kila kitu kinabadilika, jikumbushe hili kila mara ili uondokane na mazoea kwenye maisha yako.
UKWELI WA PILI; HAKUNA KINACHODUMU MILELE.
Kila kitu kinapita, kila kitu kitakuwepo kwa muda na baada ya hapo kitaondoka, hakuna chochote kitakachodumu milele. Huu ni ukweli unaopaswa kuujua na kujikumbusha mara zote. Kila kitu kinapita, hata wewe unajua kabisa kwamba hutadumu milele, unajua kabisa kuna siku utakufa, lakini je umejiandaaje kwa hali hiyo. Wengi huwa wanapenda kuukwepa ukweli huu na kuona maisha yapo na yataendelea kuwepo, na siku kifo kinawakuta wakiwa hawajajiandaa, au mbaya zaidi wanakuwa hata hawajayaishi maisha yao.
Ukweli huu unakusaidia sana kuyaishi maisha yako leo, kwa kuwa unajua kesho inaweza isiwepo, kesho ni zawadi ambayo bado hujapewa. Pia ukweli huu unakufanya utumie kitu vizuri wakati unacho, kwa sababu unajua wakati wowote unaweza kukipoteza, kwa sababu hakitadumu milele.
Chochote unachopata kwenye maisha, kuanzia uhai wako, mahusiano yako, kazi, biashara na hata mali, jua umekopeshwa kwa muda tu, kuna wakati utapaswa kurudisha na hivyo kukosa kile ulichozoea. Hivyo tumia vizuri kitu wakati unacho kwa kuwa hakitadumu milele.
SOMA; Acha Kutafuta Pesa Ambazo Hutazipata, Tafuta Hiki Kimoja Na Usahau Matatizo Yako Ya Pesa.
UKWELI WA TATU; HAKUNA KINACHORIDHISHA KABISA.
Huu ni ukweli ambao jamii imeuficha kwa wengi mno, na umekuwa chanzo cha mateso kwa walio wengi. Watu wamekuwa wanakimbizana na vitu wakiamini wakishapata wanachokimbiza basi wataridhika kabisa, watakuwa na furaha ya kudumu na maisha yatakuwa raha mustarehe. Lakini pale mtu anapopata anachokimbiza, anaona vitu vizuri zaidi ambavyo hana, na hivyo badala ya kufurahia kile alichopata, anaumizwa na kile ambacho hana.
Hakuna chochote kwenye hii dunia ambacho kitakupa hali ya kuridhika kabisa, kila kitu unachopata utaona kuna cha juu zaidi unaweza kupata. Ukiwa unatembea kwa mguu utasema ukipata baiskeli utaridhika sana. Pata baiskeli na utaona kuchochea ni tabu kwako, utaona pikipiki ni bora zaidi, hutumii nguvu zako. Pata pikipiki na utagundua usalama wako kwenye pikipiki siyo mzuri kama kwenye gari. Utaendelea hivyo na hata ukipata ndege, bado kuna kitu cha juu zaidi utaona hujapata.
Kwa kujua ukweli huu tunapaswa kupokea kile tunachopata na kukitumia huku tukiwa na utulivu. Kutokukubali kile cha juu zaidi kituvuruge na kushindwa kuthamini cha chini.
Lakini hii haimaanishi uridhike na kidogo ulichonacho na uache kutafuta vya juu zaidi, tafuta vya juu kwa sababu unaweza kuvipata, siyo kwa kukimbiza furaha, kufikiri ukishavipata basi maisha yako yatakamilika kabisa. Hakuna chochote kitakachokamilisha maisha yako kaa hujakamilika ndani yako.
Rafiki, kweli hizi tatu zimefichwa kwako miaka na miaka, tangu ukiwa mtoto mpaka leo umekuwa unatengenezewa mazingira ya kuficha kweli hizi, unaambiwa ukipata mali utakuwa na furaha, lakini unazipata na furaha hakuna. Unaambiwa usijali muda na vitu vipo, lakini siku vinapotea unaumia kwa kuwa hukuvitumia. Na wengi baada ya kupata kazi au biashara fulani, tunajiambia hatuna haja ya kusumbuka tena, lakini mabadiliko yanatokea na tunapoteza kile ambacho tuliridhika nacho.
Kila wakati badilika, tumia vizuri kila ulichonacho kama leo ndiyo siku ya mwisho kuwa nacho na jua hakuna chochote kitakachokamilisha maisha yako kama hujakamilika ndani yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge