Kuna kitu kimoja ambacho kina nguvu ya kujenga au kubomoa maisha yako.
Kitu hicho ni mahusiano yako na watu mbalimbali kwenye maisha yako.
Ubora wa mahusiano yako na wengine ndiyo ubora wa maisha yako. Yaani maisha yako yatakuwa bora kadiri mahusiano yako na wengine yanavyokuwa bora.
Utakuwa na maisha bora ya kifamilia pale ambapo unakuwa na mahusiano mazuri na wanafamilia. Pale ambapo kuna maelewano mazuri, upendo na kujali, maisha yanakuwa bora sana.
Utakuwa na maisha bora ya kikazi pale unapokuwa na mahusiano mazuri na wale unaohusika nao kwenye kazi. Mnapokuwa mnaelewana, kuheshimiana na kujaliana, kazi zinakwenda vizuri.
Kadhalika kwenye biashara zetu, zinakuwa bora kadiri mahusiano yetu na wale tunaojihusisha nao kwenye biashara hizo yanapokuwa bora. Kuanzia tunaoshirikiana nao kwenye biashara, wateja wetu na hata jamii kwa ujumla.
Kazana sana kujenga mahusiano bora kwenye kila eneo la maisha yako, kwa sababu mahusiano yakishakuwa mazuri, ushirikiano unakuwa mkubwa na chochote kinachotokea kinaweza kukabiliwa vizuri.
Kwa mfano tunajua kila familia huwa inapitia changamoto mbalimbali, sasa familia yenye mahusiano mazuri inaweza kuzivuka changamoto hizo na kubaki kuwa imara. Lakini familia isiyo na mahusiano mazuri, changamoto kidogo itawasumbua na hata kupelekea familia kuvunjika.
Mahusiano bora kwenye kila eneo la maisha yako ni kinga ya kwanza na muhimu kwa changamoto na vikwazo mbalimbali utakavyokutana navyo kwenye safari yako ya mafanikio.
Weka nguvu zako katika kuboresha mahusiano yako na utaweza kuwa na maisha bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,