Kuwa huru na kufikiri upo huru ni vitu viwili tofauti kabisa.
Watu wengi wanaojiona wapo huru, ni kufikiri kwao kwamba wapo huru ndiyo kunawapa matumaini. Lakini kwa uhalisia hawapo huru, na hawajui kama hawapo huru, kitu kinachofanya hali yao izidi kuwa mbaya zaidi.
Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kuhalalisha kila tunachofanya au kupitia kwa namna ambayo ni rahisi kwetu kueleweka. Ni katika kuhalalisha huku ndiyo tunashindwa kujua kama tuna uhuru wa kweli au fikra zetu ndiyo zinatudanganya hivyo.
Samaki huwa hajui kama yupo ndani ya maji mpaka pale anapotolewa kwenye maji hayo. Akiwa ndani ya maji anaona hayo ndiyo maisha, na hajui maji yana nguvu gani kwake. Ni mpaka pale anapotolewa nje ya maji ndiyo anagundua kwamba hakuwa huru na maisha yake, bali alikuwa akitegemea zaidi maji.
Kadhalika kwenye maisha yetu, kuna vitu tunaona ni vya kawaida kwetu, lakini ndiyo vinatunyima uhuru wetu. Ni mpaka pale tunapokosa vitu hivyo ndiyo tunagundua kwamba vilikuwa kizuizi kwetu kupiga hatua.
Wapo watu ambao wamekaa kwenye kazi au biashara fulani kwa muda mrefu, hakuna hatua ambazo wamepiga lakini wanakuwa wameridhika na mambo yanavyoenda. Kinatokea kitu ambacho kinawaondoa kwenye kazi au biashara hiyo na hapo inawabidi watafute njia mbadala, na njia mbadala wanayoipata inakuwa bora zaidi kwao kuliko walichozoea mwanzo.
Hii ni kusema kwamba dhana yetu ya uhuru siyo sahihi, vitu vingi ambavyo unafikiri upo huru, ni fikra zako ndiyo zinakupa moyo, na siyo uhuru halisi. Utajua kama upo huru pale kile ulichonacho kinapojaribiwa, pale unapokosa kile unachotegemea na kuyaona maisha ya upande wa pili.
Huwezi kusema upo huru kama umekuwa unaishi maisha yale yale ya mazoea wakati wote. Hivyo kama unataka kutengeneza uhuru wa kweli kwenye maisha yako, hatua ya kwanza ni kuacha kuishi kwa mazoea, na kila wakati kujaribu vitu vipya na vikubwa zaidi ya vile ambavyo umezoea kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,