Kikwazo cha kwanza cha mafanikio ya mtu kinaanzia ndani yake. Siyo kwenye mazingira, hali ya uchumi, kazi au biashara mtu anayopata ndiyo kikwazo, bali kikwazo kipo ndani ya mtu mwenyewe.
Watu wengi wamekwama pale walipo sasa, kwa sababu kwa ndani wameshakubaliana na hali hiyo na hawaoni picha kubwa na nzuri ya baadaye. Wengi wanaona mambo yataendelea kuwa hivyo hivyo na hakuna chochote kikubwa wanachoweza kufanya au kupata.
Sasa ukishakubaliana na mazingira, ukishakubaliana na pale ulipo sasa, maana yake umepapokea na hutasukumwa kufanya kinyume na ulivyozoea.
Njia mbadala, ambayo itakufikisha kwenye mafanikio makubwa ni kutokupokea pale ulipo sasa na kuona ndiyo njia pekee. Badala yake kuwa na picha kubwa na nzuri sana ya baadaye, ambayo unaiishi kila siku.
Kuwa na maono makubwa na mazuri sana ya baadaye, ambapo unajiona ukiwa umefanikiwa zaidi ya hapo ulipo sasa. Kisha kila siku jikumbushe picha hiyo ya mafanikio makubwa. Kwa kufanya hivi, utapata msukumo mkubwa sana wa kufanikiwa. Hutaridhika na pale ulipo sasa na hata unapopitia ugumu unajua ni kwa muda tu.
Ili kuwa na mafanikio makubwa, lazima uwe na kitu kikubwa kinachokusukuma zaidi ya pale ulipofika sasa. Acha kuishi maisha kwa mazoea na kufanya kile ambacho umeshazoea kufanya siku zote. Badala yake endesha maisha yenye utofauti, ambayo yatakuwezesha kupiga hatua zaidi. Na kitakachokuwezesha kuwa na maisha ya utofauti ni kwa kuwa na maono makubwa sana ya baadaye.
Uwezo wa kupiga hatua zaidi ya hapo ulipofika sasa tayari upo ndani yako, ni wewe kuuachilia na kuacha kujizuia ili upige hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,