Kila mtu ana sauti hasi ambayo ipo ndani yake.

Hii ni sauti ambayo kila mara inamkumbusha madhaifu yake, makosa yake, na jinsi ambavyo hawezi kufanya makubwa kama alivyopanga.

Weka mipango yoyote mikubwa na kuna kisauti ndani yako kitaanza kukusumbua, kitakuambia huwezi, kitakuonesha wengine ambao walijaribu wakashindwa.

Kuna wakati kisauti hiki kinapata nguvu kubwa na hata kuweza kuathiri ufanisi wako. Na pale unapoanza kukutana na ugumu, kitu ambacho kinamtokea kila mtu, sauti hiyo inaanza kupata ushahidi, na kukuonesha kwamba iko sahihi.

Kama haupo imara na hujajitoa kweli kufanikiwa, sauti hii iliyopo ndani yako itashinda na hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako. Na wote ambao wameshindwa, licha ya kuwepo kwa sauti za nje zilizowakatisha tamaa, lakini waliipa nafasi kubwa sauti ya ndani na hiyo kuwafanya wasiweze kupiga hatua.

Ili kuweza kuishinda sauti hii ya ndani hupaswi kupambana nayo, badala yake unapaswa kuinyima nafasi. Na njia pekee ya kuinyima nafasi ni kuwa ‘bize’ kufanya yale uliyopanga kufanya.

Unapaswa kuweka muda wako na nguvu zako zote kwenye yale uliyoanga kufanya, kila wakati uwe na kitu ulichopanga kufanya na unakifanyia kazi kweli. Akili inapokuwa imetingwa muda wote na kazi, sauti hiyo inakosa nafasi, siyo kwamba itaondoka, ila kwa kuwa akili imetingwa na mambo mengine, inakosa umuhimu.

Na kadiri unavyofanya ndivyo unavyopata matokeo mazuri na matokeo hayo yanakuwezesha kuipuuza zaidi sauti hiyo ya kukukatisha tamaa.

Adui wa kwanza wa mafanikio yako unatembea naye kwenye akili yako, ambaye ni sauti inayokukatisha tamaa iliyopo kwenye akili yako. Kama hutaweza kupuuza sauti hii na kama utakuwa na muda mwingi wa kuisikiliza, haitakuachia ufanye jambo lolote kubwa.

Mara zote kuwa ‘bize’ kuchukua hatua kwenye kile unachotaka na hutapata nafasi ya kusikiliza sauti hiyo inayokukatisha tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha